
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema sababu ya kuanza upya mchakato wa kuuza tiketi ni kwa sababu namba ya walionunua katika mchakato wa awali ni kubwa kuliko idadi ya mashabiki inayohitajika katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Amesema kuwa walionunua tiketi katika mchakato wa awali, tiketi zao zitatumika katika kilele cha siku ya tamasha la Simba Day.
“Fedha ya mtu haitopotea. Kila mtu ataitumia fedha yake wakati sahihi ukifika. Jambo kubwa lenye maana na lenye thamani kwa sasa ni ubingwa wa Afrika.
“Kwa tiketi elfu 16 ambazo zimeshauzwa maana yake Uwanja wa Amaan umeshajaa. Tunaufuta mchakato wa kuuza tiketi na tunaanza upya kuuza tiketi. Walionunua tiketi, tiketi zao watazitunza na watazitumia kuingilia katika tamasha la Simba Day.
“Jasho la mtu halipotei. Wale ambao wameshanunua tiketi, tunawaomba wazitunze tiketi zao wazitunze na itakapofika Simba Day watazitumia kuingilia uwanjani.
“Tutambue kwamba kila mtu amepata hasara kwenye hili jambo. Kwa hiyo kila Mwanasimba ipo namna ambayo ameathirika kwa hii mechi. Nini ambacho tunapaswa kufanya ni kuungana na kwenda kumshambulia adui ambaye yuko mbele yetu,” amesema Ally.
Mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika umepangwa kuchezwa Jumapili Mei 25, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10 jioni.
Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyochezwa Mei 17, 2025 katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane, Morocco, wenyeji RS Berkane waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba.