Simba yarejea kileleni Ligi Kuu

Dar es Salaam. Simba imepanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya KMC katika mechi iliyochezwa leo, Novemba 6 katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam ikifikisha pointi 25 kwenye michezo 10 ilizocheza hadi sasa.

Mabao ya Simba katika mchezo huo, yamefungwa na Awesu Awesu aliyefumania nyavu katika dakika ya 25, Jean Ahoua aliyefunga mabao mawili, moja katika dakika ya 38 lililopatikana kwa  mkwaju wa penati ambayo ilitokana na beki wa Simba, Shomari Kapombe kuchezewa vibaya katika eneo la hatari na beki wa KMC, Rahim Shomary na lingine akifunga dakika ya 68 na bao lingine moja likifungwa na  Edwin Balua katika dakika ya 66.

Mabao mawili aliyoyafunga Jean Ahoua yanamfanya kuhusika katika mabao tisa ndani ya Klabu ya Simba ambapo amefunga mabao matano na kutoa pasi nne zilizozaa mabao huku akiwa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi na Ligi Kuu kiujumla.

Awesu Awesu na Edwin Balua kila mmoja amefikisha mabao mawili kwenye Ligi Kuu baada ya kila mmoja kufunga bao moja moja. Mchezo unaofuata Simba watakuwa wageni wa Pamba Jiji kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Iliwalazimu mashabiki kusubiri kwa dakika 11 baadaye kushangilia bao la kuongoza ambalo lilifungwa katika dakika ya 24 na kiungo wake Awesu Awesu aliyeunganisha kwa shuti kali la mguu wa kulia, pasi ya Mukwala.

Shambulizi hilo lilianzishwa upande wa kulia na Ladack Chasambi ambaye alimzidi ujanja Rahim Shomary na kupiga krosi ya chinichini kwenda kwa Mukwala ambaye aliumiliki na kumpasia Awesu aliyeujaza wavuni.

Mzigo ulizidi kuwa mzito kwa KMC katika dakika ya 38 baada ya Simba kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti uliowekwa kimiani na Charles Ahoua.

Penalti hiyo ilitolewa na refa Lawi baada ya Rahim Shomari kumchezea rafu Shomari Kapombe ndani ya eneo la hatari la KMC wakati alipokuwa katika harakati za kuokoa shambulizi hilo.

Katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, KMC walipata fursa nzuri ya kufunga bao dhidi ya Simba pindi Chamou Karaboue alipomuangusha Ibrahim Elias nje kidogo ya eneo la hatari lakini Nzeyimana Jean alishindwa vyema kulenga lango na kupiga mpira huo nje.

Mabao hayo mawili ya Simba yalidumu hadi refa Lawi kutoka Kigoma alipopuliza kipyenga cha kuashiria muda wa mapumziko.

Robo saa baada ya kipindi cha pili kuanza, Simba walifanya mabadiliko ya kuwatoa Debora Mavambo na Awesu Awesu ambao nafasi zao zilichukuliwa na Edwin Balua na Mzamiru Yassin.

Edwin Balua alitumia dakika sita tu baada ya kuingia kuifungia Simba bao la tatu kwenye mchezo huo baada ya kumalizia kwa shuti kali la mguu wa kushoto, pasi ya Valentine Nouma aliyeonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.

Sherehe ya mabao kwa Simba ilihitimishwa katika dakika ya 69 na Charles Ahoua aliyetumia vyema makosa ya beki Ismail Gambo aliyeteleza wakati alipokuwa katika harakati za kuokoa pasi ndefu iliyopigwa na Fabrice Ngoma kutoka katikati ya uwanja.

Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena hapo kesho, Novemba 7  ambapo mabingwa watetezi Yanga watakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Azam Complex kuwakaribisha Tabora United.

KMC kwa kufungwa leo, imejikuta ikibakia katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Kwenye mechi ya leo, Simba iliwatoa pia Fabrice Ngoma, Ladack Chasambi na Chamoue Karabou ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hussein Kazi, Kibu Denis na Omary Omary.

KMC yenyewe iliwatoa Ibrahim Elias na Redemptus Musa ambao nafasi zao zilichukuliwa na Fred Tangalo.