Simba yapewa mwamuzi mwenye rekodi zake

KATIKA hesabu za Simba kuhakikisha inachanga vizuri karata zake na kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, inatakiwa kuwa makini na mwamuzi wa mchezo wao wa marudiano kutokana na rekodi zake zilivyo.

Simba ambayo Aprili 9 mwaka huu itakuwa mwenyeji wa Al Masry katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, inahitaji ushindi wa tofauti ya mabao matatu ili kufuzu kufuatia kufungwa 2-0 ugenini.

Sasa katika kuamua hatma yao hiyo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limempanga mwamuzi Djindo Louis Houngnandande, raia wa Benin, kuchezesha mechi hiyo.

Mwamuzi huyo aliyezaliwa Agosti 25, 1985 akiwa na umri wa miaka 39, rekodi zinaonyesha amechezesha jumla ya mechi 31 za mashindano tofauti ya CAF ambapo ngazi ya klabu ni 16 pekee. Katika mechi zote 31, ametoa jumla ya kadi 122, wastani wa kadi 3.9 kwa mechi, kati ya hizo 119 za njano na tatu nyekundu. Pia mwamuzi huyo katika mechi hizo 31 ametoa penalti 10.

Mara ya mwisho mwamuzi huyo kuchezesha mechi iliyohusisha timu ya Tanzania na ya Misri ilikuwa Machi Mosi, 2024 katika mchezo wa mwisho wa Kundi D kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Al Ahly ikiwa nyumbani iliifunga Yanga bao 1-0.

Januari 21, 2024, alichezesha mechi ya Kundi F kwenye michuano ya AFCON iliyofanyika Ivory Coast wakati Tanzania ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia.

Pia Februari 12, 2023, alichezesha mechi ambayo US Monastir kutoka Tunisia ilipoifunga Yanga mabao 2-0 kwenye Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika.

Kuanzia Desemba 8, 2019 alipoanza kuchezesha mashindano ya CAF ngazi ya klabu, ni timu mbili tu za ugenini zilipata ushindi pindi alipochezesha mwamuzi huyo ambayo ni Jaraaf ya Senegal iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Salitas ya Burkina Faso, Aprili 12, 2021 na Al Hilal ya Sudan iliyoichapa MC Alger 1-0, Desemba 14, 2024. Kwa upande wa timu za nyumbani wakati mwamuzi huyo akichezesha, 13 zimeondoka na ushindi huku sare ikiwa ni moja pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *