
Wadau na mastaa wa soka nchini wameipa Simba mbinu ili iweze kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa pili wa marudiano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Berkane, utakakaopigwa Mei 25, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.
Simba imebakiza saa 48, kabla ya kuingia uwanjani kutafuta rekodi mpya ya soka Tanzania, keshokutwa Jumapili.
Huu ni mchezo wa pili wa fainali baada ya ule wa kwanza kupigwa Morocco na Simba kulala kwa mabao 2-0, hivyo inatakiwa kupata ushindi wa mabao 3-0 au zaidi ili kutwaa ubingwa huo wa pili kwa ukubwa kwenye soka Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, ametoa zawadi maalumu kwa timu hiyo kwa kusema kuwa atagharamia matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex na atakuwa mmoja wa watakaohudhuria uwanjani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mastaa wa zamani wa soka nchini Tanzania, wamesema kuwa Simba wanatakiwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa wageni wao hawapati mabao ya mapema.
mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emanuel Gabriel alisema kocha wa Simba, Fadlu Davids alikuwa sahihi kumuanzisha Leonel Ateba ugenini, kutokana na uwezo wake wa kukaa na mpira mguuni, kushambulia na mikimbio iliyo sahihi, lakini anaweza akapanga kikosi kwa mfumo wa 4-4-2 ama kikacheza kikosi kilekile.
“Steven Mukwala ana kasi na mikimbio mizuri isipokuwa anashindwa kukaa na mali mguuni, tofauti na Ateba anaficha mpira mguuni, lakini sina shaka na kikosi kilichoanza ugenini kinaweza kikaanza na hapa pia, kocha ndiye anajua nani kaamka vizuri na kama mchezaji anaumwa aseme mapema ili isitokee kama yale ya Abdulrazak Hamza.
“Wachezaji wa Simba wajitolee kupambania nchi, wasicheze kama wapo kazini kuchukulia kirahisi kama wakifungwa sawa wakishinda sawa, hiyo mechi ni ya kihistoria, naamini kuna uwezekano mkubwa wakapata mabao matatu kulingana na kile ambacho walikionyesha kipindi cha pili wakiwa ugenini.”
Wakati akisema hivyo, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na timu ya Tanzania ‘Taifa Stars, Steven Mapunda ‘Garincha’ alisema ili kupata matokeo ya haraka kipindi cha kwanza kocha Fadlu amuanzishe Kibu Denis, Joshua Mutale, Elie Mpanzu namba tisa kama wote watakuwa fiti Mukwala aanze na Ateba aingie kipindi cha pili.
“Fadlu alikuwa sahihi kumchezesha Ateba ugenini ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kuondoka na watu kama watatu hadi wanne, hivyo wapinzani walikuwa wanaogopa kupanda juu, hao niliowataja Mutale, Kibu, Mpanzu na Mukwala wakianza kipindi cha kwanza wana uwezo wa kupata matokeo ya mabao mawili, ili kina Ateba wakiingia kipindi cha pili watafute bao la ushindi,” alisema na kuongeza,
“Mabadiliko hayo yatategemeana na mazoezi ya mwisho ya kujua mchezaji gani yupo fiti, ukiachana na nafasi ya mbele kunatakiwa umakini mkubwa eneo la kujilinda.”
Mbali na wachezaji hao, kocha wa Asec Mimosas ambaye timu hiyo ilipoteza dhidi ya Berkane hatua ya robo fainali, amesema Fadlu anatakiwa kujidhatiti kwenye eneo la kujilinda, pia aanze mechi kwa kasi na sio kama ugenini.
“Hii ni mechi ya nyumbani, tayari umeshapoteza ugenini unatakiwa kuwa makini kwenye kujilinda, lakini kocha aanze mechi hiyo kwa kasi ya hali ya juu ili kutafuta mabao ya mapema, lazima apange wachezaji ambao wanaweza kumpa mabao ya mapema.
“Hii ndio mbinu pekee ambayo inaweza kuwapa ushindi kwenye mechi hiyo, lakini wakiruhusu mapema shida itaanza,” amesema kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika.
Mo awapa mzuka
Rais wa heshima wa klabu ya Simba, Mohamed ‘MO’ Dewji, jana alitoa kauli nzito kuhusiana na mechi hiyo kupelekwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, huku akiwahamasisha Wanasimba kwamba mnyama atanguruma popote na Jumapili itabeba ndoo.
“Sisi Simba kucheza New Amaan Complex kwa mtazamo wangu binafsi hatukutendewa haki, Tunaenda Zanzibar si kwa hiari yetu bali kwa wajibu na tutatimiza wajibu huo,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza;
“Kwa wachezaji wetu mnaovaa nembo yenye historia ingieni New Amaan vichwa juu chezeni kwa ujasiri kwa umakini na kwa utulivu kama mashujaa wa Simba mlivyo.”