Simba imepanga kumaliza mzimu wa sare ambao umeitesa kwa siku 1363 dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi kwa kupata ushindi katika mechi baina yao kesho Jumatano, Februari 19,2025.
Tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1, Mei 29, 2021 uwanjani hapo, Simba imeshindwa kufurukuta tena dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa baada ya kutoka sare katika mechi tatu zilizofuata baina yao uwanjani hapo.
Katika msimu wa 2021/2022, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na msimu uliofuata wa 2022/2023 mechi baina yao katika Uwanja wa Majaliwa ikaisha kwa sare ya bao 1-1.
Msimu uliopita, Simba ilipoenda tena kwenye Uwanja wa Majaliwa, ililazimishwa sare ya mabao 2-2.

Beki wa Simba, David Kameta ‘Duchu’ amesema kuwa hawafurahishwi na jinsi wanavyoangusha pointi wakiwa Ruangwa dhidi ya Namungo FC na mechi ya kesho wataitumia kuondoa jinamizi hilo.
“Sisi wachezaji wa Simba tumejiandaa vizuri kwa mchezo, maandalizi yapo vizuri. Kweli katika mechi za nyuma, hatujaweza kupata matokeo mazuri katika uwanja huu tunajua hilo.
“Huu ni mchezo mwingine na siku nyingine na ukiangalia pia mwalimu ni mwingine na wachezaji ni tofauti kwa hiyo sisi akili yetu ni kupata ushindi,” alisema Duchu.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema amepata muda mwingi wa kuandaa mbinu za kukabiliana na Namungo.
“Mechi dhidi ya Dodoma ambayo iliahirishwa imetupa muda zaidi wa kujiandaa. Maandalizi yetu yameenda vizuri. Tunaiandaa hii mechi dhidi ya kocha mzuri sana.
“Namungo sasa ni timu nzuri sana inayofundishika na imepangiliwa vyema kwenye ulinzi hivyo tunapaswa kuwa bora. Tunaenda kushambulia lakini wakati huohuo kuwazuia,” alisema Fadlu.

Kocha wa Namungo, Juma Mgunda alisema kuwa wapo tayari kushindana na Simba.
“Tunamshukuru Mungu wachezaji wako vizuri na leo wameamka vizuri na hiyo inaonyesha kuwa Mungu yuko nasi. Ni mechi ambayo ina umuhimu wake. Maandalizi yote ya kucheza mechi nzuri kama hiyo yamekamilika.
“Wachezaji ambao walikuwa majeruhi wako vizuri. Ni mechi ambayo ina mahitaji tofauti lakini yanayofanana. Tunaombea wachezaji waamke salama kesho ili kila mmoja akatimize wajibu wake,” alisema Mgunda.

Ushindi kwa Simba kwenye mechi hiyo utaifanya iendelee kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 50.
Kwa Namungo ushindi katika mechi hiyo utaifanya ifikishe pointi 24.