Simba, Yanga zinavyolijenga, kulibomoa soka la Tanzania

Dar es Salaam. Habari ya mjini ni mvutano unaoendelea baada ya mechi ya watani Simba na Yanga kuahirishwa siku ya mchezo, Machi 8, mwaka huu.  Kamati ya Uendeshaji na usimamizi wa Ligi Kuu Bara (TPLB) saa 7:53 mchana ilitangaza kuahirisha mchezo huo uliopagwa kuchezwa saa 1:15 usiku wa siku hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Vuguvugu la kutochezwa kwa mechi hiyo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara lilianzia kwa Simba kutoa tamko usiku wa kuamkia siku ya mechi, ikieleza kuwa haitapeleka timu uwanjani kufuatia msafara wa kikosi chake kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 17(45) za Ligi Kuu Bara, timu mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika, lakini Simba walipofika uwanjani hapo walizuiwa kuingia.

Hata hivyo, taarifa ya Bodi ya Ligi ya kuahirisha mchezo huo iliyotolewa mchana wa Machi 8, mwaka huu, ilieleza dosari kadhaa ikiwemo klabu ya Simba kutofanya mawasiliano na timu mwenyeji, msimamo wa uwanja na mkuu wa usalama wa mchezo huo kueleza kwamba, wanakwenda uwanjani kufanya mazoezi.

Sababu hizo zinatajwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyosababisha sintofahamu na hatimaye mchezo huo kutofanyika. Yanga kwa upande wake, iliweka msimamo kwa kupeleka timu uwanjani na kufuata taratibu zingine kama zinavyotakiwa.

Pia, imeeleza kuwa hatashiriki mchezo mwingine baina yake na Simba kwa msimu huu kwa kuwa, kanuni za kuahirishwa kwa mchezo huo hazikufuatwa.

Baada ya mzozo huo, Bodi ya Ligi licha ya kutangaza kuahirishwa kwa mchezo huo, pia imeeleza kuwa itafanya uchunguzi zaidi ili kutoa uamuzi wa haki ikisema itatoa taarifa kamili ya tukio hilo sambamba na kutangaza tarehe ya mchezo huo.

Jumapili ya Machi 9, mwaka huu, Yanga ilitoa taarifa usiku baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji iliyokutana kwa dharura, ikisema haitakubali kurudiana na Simba kufuatia mchezo wao wa Machi 8 kuzuiwa na Bodi ya Ligi.

Hata hivyo, tukio hilo ni miongoni mwa mengi yanayozihusisha Simba na Yanga yanayoacha maswali, yanayochochea kanuni kupindishwa na zaidi yakitajwa kuwa na harufu ya kulibomoa soka la Tanzania licha ya mchango mkubwa wa timu hizo kwenye ujenzi wa soka.

Mwananchi Digital imefanya mahojiano na baadhi ya waliowahi kuwa watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa nyakati tofauti, Celestine Mwesigwa na Angetile Osiah ambao, wameeleza kuwa Yanga na Simba ndio zimeshikilia hatma ya soka la Tanzania.

“Ni timu kubwa na maamuzi yoyote dhidi ya hizi huwa na gharama kwenye mpira na hata zaidi ya mpira wenyewe,” anasema Mwesigwa akizungumzia zaidi kuhusu klabu hizo zenye mashabiki wengine zaidi nchini, hasa zinapokutana au kuwepo kwa uamuzi unaotakiwa kufanywa kuzihusu,

Mwesigwa amesema presha huwa kubwa kwa watendaji. “Ilikuwa kuna jambo lao, au hata ziwe zinacheza basi simu zinapigwa sana, wakati mwingine hadi na watu wazito kwa kuwa ni timu zenye nguvu,” amesema.

Amesema nguvu iliyopo kwenye timu hizo ndizo zinazifanya kuendelea kuwa kubwa, na zinapofanya vizuri na Ligi kuwa bora kunachangizwa na uwekezaji unaozihusu zenyewe zaidi.

Kuhusu tukio la kuahirishwa mechi ya Machi 8, mwaka huu, Mwesigwa amesema ni la aibu na kama halitachukuliwa hatua na huenda likapoteza imani ya mashabiki na kupunguza hamasa yao kwenda uwanjani na hata kupunguza wawekezaji kwenye soka.

“Hili sio tukio ambalo linazungumzwa Tanzania pekee, hadi mataifa mengine ya Afrika linazungumzwa sana. Ni aibu na linaweza kusababisha soka letu kuporomoka, vyombo husika visiliangalie tu kwa kutoa maamuzi lakini watafute suluhisho ili lisijirudie tena,” amsema Mwesigwa.

Amesema Ligi Kuu Bara imekuwa maarufu zaidi Afrika kutokana na watu kuiamini na kuweka pesa zao, Yanga na Simba kwa sasa zimeshikilia hatma ya ubora hivyo, zinapofanya makosa ya aibu zinaondoa imani kwa mashabiki na wawekezaji.

“Hiki kilichotokea kinatakiwa kipate tiba, Bodi (TPLB) iliahirisha mchezo, tunasubiri iseme nani amesababisha mechi ivunjike. Kwenye hili suala kanuni zipo, swali ni je? Kanuni hizo zimejitosheleza na kama zimejitosheleza hatua gani zichukuliwe. Siku zote hakuna maamuzi yasiyokuwa na lawama, presha za Simba na Yanga zipo, lakini kinachotakiwa ni maamuzi wenye weledi na haki,” ameongeza.

Kwa upande wake, Osiah amesema presha kwenye kwa Simba na Yanga huwa kubwa pale inapotokea mojawapo inapaswa kupewa adhabu akitolea mfano wa tukio la kuahirishwa kwa mchezo huo na timu inayostahili kupewa ama kukatwa alama.

“Presha yake itakuwa kubwa pale hizo pointi tatu Yanga wakipewa, halafu mwisho wa msimu ikawa Simba inahitaji pointi tatu tu ili iwe bingwa, hapo shughuli yake itakuwa nzito sana,” amesema Osiah.

Amesema kama kanuni zinafuatwa na kuzingatiwa suala la kuwa na presha halipo huku akieleza kuwa kwa kosa la timu kutotokea uwanjani kwenye mechi, adhabu yake ni kushushwa daraja.

“Japo kwenye ili hatuwezi kusema Simba imekosea kwa kutotokea uwanjani kwa kuwa Bodi ilitoa taarifa ya kuahirishwa mechi kabla ya muda wa mechi,” amesema.

Je adhabu kuzingatiwa ?

Baadhi ya wadau wa soka kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia uamuzi sahihi unaopaswa kuchukuliwa dhidi ya Simba na Yanga pindi zinapopindisha kanuni huku wengine, wakizipa majina ya ‘watoto pendwa wa TFF.

“Nakumbuka Simba iliwahi kunyang’anywa pointi tatu kule Kagera, kuna mwaka pia ilipitishwa kanuni mchezaji anayetumikia kadi tatu za njano anaweza kuamua adhabu yake iwe katika mechi zipi, Simba iliitumia ikaleta kelele, haikudumu muda mrefu ikaondolewa.  Lakini, tukisimama kwenye kanuni, hakuna kitakachoharibika,” amesema Mwesigwa.

Kwa Osiah yeye katika adhabu ameanza kwa kutolea mfano miaka ya nyuma ambapo Yanga iliwahi kufungiwa miaka mitatu kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati na aliyekuwa bosi wa Cecafa, Leodger Tenga.

“Hakuna presha kama utaziadhibu Simba ama Yanga kwa kufuata kanuni, na hapa inahitaji kiongozi mwenye msimamo na anayesimamia kanuni,” amesema Osiah.

Kuhusu adhabu hiyo iliyotolewa na Cecafa, Osiah amesema Yanga iligoma kucheza na Simba mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, baada ya timu hizo kutolewa kwenye nusu fainali.

“Yanga walizua tu hoja kuwa hadi walipwe Sh30 milioni ndipo wataingiza timu uwanjani, nilimuuliza Kondic (Dusan aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga wakati ule) akaniambia kila mchezaji aliyekuwa akizungumza naye kuhusu mechi ile alisema ni mgonjwa,” amesema.

Hata hivyo, Osiah amesema kuwa adhabu hiyo badala ya miaka mitatu utekelezaji wake ulikuwa wa miaka miwili pekee kwani, mwaka uliofuatia, mashindano hayo yalifanyika nchini na Yanga wakapata nafasi ya kushiriki.

Athari zake katika soka

Nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mtemi Ramadhani amesema matukio ya Simba na Yanga hayana afya katika soka la Tanzania.

“Sheria na kanuni zipo, inapotokea timu inazivunja makusudi inasikitisha sana. Hawajui kama watu wanapoteza gharama zao kuja kutazama mechi?,” anahoji Mtemi.

Anasema pindi Simba na Yanga zinapocheza mashabiki wanatoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya mchezo huo, hivyo kuahirishwa kwa sababu nyepesi kunapunguza hamasa na kutia doa soka la Tanzania.

“Ili tusifike kubaya, mamlaka zitoe adhabu kali kwa wakosaji, tusiogopane fulani hakutokea kwenye mechi sheria inasemaje. Sheria na kanuni hizi zisitekelezwe kwa Gwambina, Mashujaa ama Mtibwa Sugar bali iwe kwa yoyote,” anasema huku akigusia wakati wa Tenga akiifungia Yanga miaka mitatu kushiriki michuano ya Cecafa.

Kuhusu vurugu za kuahirishwa kwa Kariakoo Derby, Mtemi amesema pamoja na Yanga kukosea kwa kuizuia Simba kufanya mazoezi, Simba nayo haikupaswa kugomea mechi bali walitakiwa kuwasilisha malalamiko TFF na Bodi ya Ligi na sio kugoma kucheza.

Nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay amesema mechi kutangazwa kuahirishwa siku ya mechi huwa inatokea kwa sababu za msingi hasa zinazohusu usalama.

“Inashangaza hiki kilichotokea Jumamosi (Machi 8) kwa kuwa Bodi ndiyo yenye mamlaka na ndiyo ilitangaza kuahirisha mechi, tusubiri ituambie sababu, madhara na adhabu kwa wahusika,” anasema Mayay ambaye amepata kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Taifa Michezo (BMT).

Makucha ya TFF yanavyosubiriwa

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF (wakati huo Chama cha Soka), Ismail Aden Rage amesema katika haya yanayotokea kwa Simba na Yanga, TFF inapaswa kuonyesha makucha na mamlaka yake.

“Kuna hawa watu wanajiiya mabaunsa kazi yao ni nini? Serikali ina polisi, ina JKT lakini bado hawa mabaunsa wanajipenyeza kwa ajili ya kitu gani, TFF isiruhusu huu ugonjwa wa watu kulinda uwanja ni kujidanganya,” amesema Rage.

Amesema hakuna ubishi kuwa Tanzania klabu kubwa ni Simba na Yanga, hivyo kutoa uamuzi unaozihusu inahitajika akili kubwa, haki na uwazi kutumika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *