Simba, Yanga na mabenchi ya kisasa

Klabu ya Yanga hivi karibuni ilimtambulisha kocha wake mpya Saed Ramovic kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi ambaye amefungashiwa virago baada ya kukaa Jangwani zaidi ya mwaka mmoja.

Ramovic raia wa Ujerumani anapewa nafasi kubwa ya kuipeleka Yanga katika nchi ya ahadi kutokana na mbinu zake, ujuzi na misimamo kwenye falsafa zake za soka duniani.

Hata hivyo,  kitendo cha Yanga kumleta kocha huyo siyo tu kwa kuwa ni bora mwenye kufundisha bali wanakwenda na dunia inavyotaka kwa sasa.

Dunia ya sasa ya soka haina tofauti kubwa sana na matumizi ya kompyuta, simu au vifaa vingine vya umeme ambavyo vimekuwa vikibadilika kila kukicha, hivyo ndiyo soka linavyobadilika dunia nzima na kama Yanga wangebaki kwa Gamondi basi ilikuwa rahisi kuamini kuwa wanashindwa kwenda na mwenendo na mabadiliko ya teknolojia.

Lakini pia hauepuki kwa sasa kusema kuwa timu hiyo ya Jangwani, imehama na kuwafuata wapinzani wao Simba ambao walishtuka mwanzoni tu mwa msimu na kuhama kutoka zama za kale na kuhamia kwenye zama za sasa.

Dunia ya sasa inahitaji makocha vijana wenye ujuzi wa hali ya juu, lakini wenye elimu mpya ya soka la kisasa ndiyo maana ni rahisi kwao kwa sasa kubadilisha baadhi ya mbinu ambazo zilikuwa zinatumika miaka kadhaa nyuma na kuleta mifumo mipya.

Mbinu za makipa kutumika kama nyongeza ya mabeki wa kati, kutumia zaidi miguu kuliko mikono ni za makocha wa kisasa, zaidi wakitajwa kina Pep Guardiola ambaye alikabidhiwa timu akiwa na miaka 39 tu, lakini pia mfumo wa kuwatumia mawinga kama mabeki wa pembeni, mabeki wa pembeni kama mawinga nao ulikuwepo lakini kwa sasa ndiyo umekuwa ukitumiwa zaidi kutokana na makocha hawa kufahamu jinsi ya kuwapa majukumu vizuri, kutokana na mabadiliko ya elimu ya kila siku.

Kwa miaka ya hivi karibuni, hii ni mara ya kwanza timu za Simba na Yanga zinaamini kwa makocha vijana wenye miaka 45 kushuka chini, kitu ambacho miaka 15 nyuma wasingeweza kufanya hivyo kwa kigezo kuwa hawana uzoefu, ni watoto wadogo, lakini kwa kuwa dunia imewafundisha hakuna namna tena wanalazimika kupitia njia za wakubwa wao.

Fadlu Davids

Ni rahisi kuamini kuwa huyu alikuwa wa kwanza kutoka nje ya nchi kuaminiwa na timu kubwa ya Simba  Pamoja na kuwa na umri wa miaka 43  tu, lakini akapewa timu hiyo yenye ndoto kubwa na tayari ameshaonyesha kuwa kazi hiyo anaifahamu tena kwa kutumia wachezaji wengi vijana ambao hawana uzoefu mkubwa kwenye soka.

Mashabiki wa Simba tayari wana furaha baada ya kocha huyo kuiongoza timu kwa michezo 10 tu, lakini ameshashinda minane, ametoka sare mmoja na kupoteza mmoja tu tena dhidi ya Yanga ambayo inatajwa kuwa timu kubwa hapa nchini.

Umri wa kocha huyo unaenda na kikosi chake, lakini wasaidizi wake, ambapo  wa kwanza Darian Wilken ana miaka 30 tu, akiwa amezaliwa mwaka 1994,  lakini pia Riedon Berdien  ana miaka 42 tu akiwa ni kocha wa viungo wa timu hiyo, changanya na kina Seleman Matola mwenye miaka 46 na Meez Kajee, hakuna hata mmoja aliyefikisha miaka 49 kwenye benchi la timu hiyo ambayo inatafuta kwa nguvu kubwa nafasi ya kufanya vyema kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mmoja kati ya mtu wa karibu na benchi hilo, anasema kuwa wageni hao wamekuwa wakitumia muda mwingi kusoma wapinzani, kusoma kozi ndogondogo kwenye mitandao kila siku na nia adimu kwao kuwaona wamelala kabla ya saa sita usiku na huamka kabla ya saa 12 kamili asubuhi kila siku na kuanza kufanya mazoezi binafsi.

“Hawa jamaa wanatoa elimu kubwa sana, kwanza wanatembea na mashine yao ya kutengeneza kahawa kila mahali, wanafanya kazi hadi usiku sana ni ngumu kuwaona wakiwa wamekaa hawana kazi, kama hawafundishi basi elewa kuwa watakuwa kwenye kompyuta zao muda mwingi wakifanya kazi zao, wakisoma na wakati mwingine wamekuwa wakitazama mikanda na wapinzani na kujadiliana baadhi ya mambo, ukweli ni makocha wa kisasa.

“Kushtuka usiku na kukutana wamekaa wanafanya kazi ni jambo la kawaida sana kwao, lakini jambo lingine kubwa wanasikilizana sana na kila mmoja anaheshimu kazi ya mwenzake,” kilisema chanzo hicho.

Saed Ramovic

Huyu ni kocha mwingine kijana ambaye ameaminiwa na Yanga ambayo inataka kufanya kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bosi wa benchi lao la ufundi ana miaka 45 tu akiwa kama alivyo Fadlu wa Simba, hana historia kubwa kwenye soka duniani akiwa ameifundisha timu moja tu Tx Galaxy ya Afrika Kusini tena kwa misimu miwili tu, siyo kosa kwake kwa kuwa makocha wengi wakubwa duniani walianza kupata mafanikio makubwa wakiwa hawana rekodi kubwa huko nyuma.

Kama ilivyo kwa Simba, msaidizi wa Ramovic ni Mustafa Kodro mwenye miaka 43 tu, akiwa nyuma ya bosi wake kwa miaka miwili, Mkurugenzi wa Ufundi ni mwenye miaka 43, hivyo ni sahihi sasa kuamini kuwa soka la kisasa limewahi kwa vijana na mwendo huo ndiyo wanaufuata Simba na Yanga.

Kulaumu kuwa Simba au Yanga ina makocha ambao hawana uzoefu kwenye soka hakuna hoja, kama utakuwa unakubali kuwa Mikel Arteta alienda Arsenal moja ya timu kubwa duniani akiwa anatokea kuwa msaidizi wa Pep Guardiola wa Man City akiwa hakuwahi kuifundisha timu yoyote kubwa, Arsenal walimuona wapi akifundisha zaidi ya kuwa nyuma ya Guardiola nafikiri hakuna na hata mashabiki wengi duniani walishangaa?

Lakini pia mwanzilishi wa soka la kisasa Pep raia wa Hispania  hakupata mafanikio baada ya kufundisha timu kubwa bali alianza kuifundisha Barcelona akitokea kwenye timu ya vijana ya kikosi hicho La Masia  akaenda timu kubwa akiwa na umri usiozidi miaka 35, kilichobaki kwa sasa ni historia na dunia nzima inatambua alichofanya.

Arteta ambaye anasumbua kwenye soka duniani kwa sasa usifikiri ni mkongwe huyu ni kocha mwenye miaka 42 tu akiwa alijiunga na Arsenal na miaka 39, lakini alitengeneza benchi la ufundi la kufanana naye kama ambavyo wanafanya Fadlu upande wa Simba na Ramovic upande wa Yanga.

Manchester United ni klabu yenye ushawishi mkubwa duniani ilikuwa inaweza kumchukua kocha yoyote mwenye wasifu mkubwa kwenye soka kwa sasa lakini ilimtazama Ruben Fillipe Marques Amorim akitokea nchini Ureno bila kuwa na pilika pilika nyingi za soka la ushindani tena akiwa na miaka 39 tu anakwenda kuiongoza klabu kubwa kama Man United ambapo aliyeondoka ni Erik ten Hag mwenye miaka 54, lakini pia tazama aliyekaimu nafasi yake Ruud Van Nisterooy bado ni kijana mdogo mwenye miaka 48 tu kwa sasa.

Unaweza kuamini kuwa Liverpool inafundishwa  na Arne Slots ambaye ana miaka 46 tu? Na tayari ameshaweka rekodi kadhaa kubwa ambazo zilishindikana kwenye kikosi hicho, kama huamini kuhusu project ya Yanga, basi waulize Liverpool walimpata wapi kocha huyo akiwa ameanza kufundisha soka kuanzia mwaka 2017 tu.

Kwa Afrika Mamelodi ni waumini wazuri wa makocha hawa vijana na walichofanya kwa Rolan Mokwane akiwa na miaka 33 kila mmoja alikiona, sawa projekti yao haikutimia lakini tayari ameshaionyesha dunia ubora wake na yupo kwenye timu kubwa Afrika Wydad Casablanca.

Hakuna ubishi kuwa walichokifanya Simba waliangalia wakubwa kwenye soka duniani wamefanya nini, Yanga nao wakaja kwenye njia hiyohiyo, tusubiri tuone kama wengine watafuata lakini hakuna ubishi kushinda na kocha mwenye umri mkubwa kwa sasa ambaye hatembei na mashine ya kutengeneza kahawa ni kazi ngumu sana.