
MABINGWA watetezi wa wa Kombe la Muungano, Simba wanatarajia kushiriki mashindano hayo yanayotarajia kuanza Aprili 21 hadi 27, mwaka huu, Zanzibar.
Mbali na Simba, timu nyingine kutoka Bara zinazotarajia kushiriki mashindano hayo ni Yanga, Azam na Coastal Union, huku Zanzibar ikiwakilishwa na JKU, KMKM, KVZ na Zimamoto.
Mashindano hayo yanatarajia kushirikisha timu nne kutoka Bara na nne Zanzibar tofauti na msimu uliopita ambapo Simba ndio ilitwaa ubingwa wa michuano iliyoshirikisha timu nne zikiwamo Azam, KMKM na KVZ.
Simba ilitwaa taji la michuano hiyo iliyorejea tena baada ya kutofanyika kwa takriban miaka 22 tangu mara ya mwisho ilipoacha kuchezwa 2002 na kuzawadiwa Sh50 milioni, huku Azam iliyomaliza ya pili ikizoa Sh30 milioni.
Ligi hiyo ilianza 1982 kwa lengo la kudumisha Muungano ambao mwaka huu unafikisha miaka 60 tangu ulipoasisiwa Aprili 26, 1964 ili kutoa usawa wa kiuwakilishi katika michuano ya kimataifa ya klabu za Bara na Zanzibar.
Michuano hiyo ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo ikishuhudia timu tisa zikiibuka na kombe hilo katika miaka tofauti.