Simba yaishusha Yanga kileleni, yaifumua Tabora United

NYUKI wa Tabora leo  wametulizwa nyumbani baada ya kufumuliwa tena mabao 3-0 na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara na kuhitimisha tambo ilizokuwa nazo timu hiyo mbele ya vigogo, ikithibitisha unyonge uliopitiliza dhidi ya Mnyama kwa kufungwa jumla ya mabao 12-0 katika mechi nne walizokutana katika ligi kuanzia msimu uliopita.

Tabora ilionekana tishio baada ya kuifunga Yanga kwa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam, kisha kuizima Azam kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kwa mabao 2-1 na kutoka sare ya Singida Black Stars timu zilizopo katika Nne Bora ya Ligi Kuu kwa msimu huu, lakini Simba imeonyesha kuwa ni maji ya shingo kwa nyuki hao wa Tabora.

Ikitembeza boli lenye ufundi na kasi, Simba iliizima Tabora kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kuendeleza ubabe mbele ya wenyeji wao hao ambao tangu wapande Ligi Kuu Bara walikuwa hawajawahi kuonja ushindi wowote ama sare mbele ya Mnyama.

Msimu uliopita Tabora ilianza kwa kipigo cha mabao 4-0 nyumbani kisha kulala ugenini 2-0, wakati kwa msimu huu ilikubali kichapo cha 3-0 ugenini kabla ya leo tena kukubali kipigo hicho cha cha 3-0 nyumbani kilichoirudisha Simba kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi 43 ikiing’oa Yanga yenye alama 42.

Shukrani ya ushindi wa leo zinaenda kwa Leonel Ateba aliyewanyamazisha Nyuki wa Tabora mapema kwa kufunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza kabla ya beki Shomari Kapombe kuongeza jingine na kumfanya beki hiyo kufikisha jumla ya mabao matatu hadi sasa wakati Ateba naye akifikisha saba.

Huo unakuwa ni ushindi wa 10 mfululizo kwa Simba katika ligi tangu ilipopoteza dhidi ya watani wa jadi, Yanga kwenye pambano la Dabi ya Kariakoo lililopigwa Oktoba 19 mwaka leo  baada ya beki wa timu hiyo, Kelvin Kijili kujifunga katika harakati za kuokoa mpira langoni mwake.

Mziki uleule

Kocha wa Simba Fadlu Davids hakubadilisha kitu chochote kwenye kikosi chake kilichocheza mechi tatu zilizopita za Kombe la Shirikisho Afrika, ikitumia mfumo uleule wa 4-2-3-1.

Ateba, Mpanzu waibeba

Simba haikuwa na kazi kubwa sana kipindi cha kwanza ikitawala mchezo na kutengeneza mabao mawili ya haraka kupitia mshambuliaji wake Lionel Ateba aliyefunga mara mbili dakika za 12 kwa shuti kali na lile la penalti dakika ya 34, yakitosha kuipeleka mbele ndani ya dakika 45 za kwanza.

Mabao yote hayo mpishi alikuwa Ellie Mpanzu aliyetoa asisti ya bao la kwanza kisha kutengeneza penalti baada ya kuangushwa kwenye eneo la hatari na Ateba akifunga la pili na la tatu la Shomari Kapombe.

Tabora hoi 45 za kwanza

Tabora haikuonyesha kuitaka mechi, ikitumia muda mwingi kucheza katika eneo lake na kuiacha Simba kutawala kwa kila aina ya takwimu ambapo ilimaliza dakika 45 za kwanza ikipiga shuti moja lililolenga lango.

Angalau kipindi cha pili ambacho Tabora ilirudi ikifanya mabadiliko mawili ikimtoa Cedric Martial nafasi yake ikichukuliwa na Asiegbu Shedrack lakini pia akitolewa Banele Junior nafasi yake ikienda kwa mshambuliaji mpya Joseph Akandwanaho.

Mabadiliko hayo angalau yaliongeza uhai kwa Tabora na kuonekana ikija mbele na kupandisha mashambulizi na kuwashambulia wageni wao lakini hata hivyo mashambulizi hayo yaliishia kwenye mikono ya kipa Moussa Camara aliyeokoa kibabe mashuti yao.

Ateba amfuata Ahoua

Mabao hayo mawili ya Ateba yanamfanya kufikisha mabao saba kwenye msimamo wa ufungaji akimfikia mwenzake Charles Ahoua, sambamba pia na Clementi Mzize, huku Pacome Zouzoua na Selemani Mwalimu aliyekuwa Fountain Gate aliyetimkia Wydad Casablanca, wakifuata wakiwa na mabao sita kila mmoja, huku juu ya wote kinara akiwa ni Elvis Rupia mwenye mabao manane.

Simba pointi, Tabora pesa

Simba imeondoka na pointi zote tatu na mabao matatu lakini Tabora haikuachwa hivihivi, imeachiwa fedha za kutosha kufuatia uwanja huo kufurika mashabiki ambao ni wazi utawafuta jasho wenyeji kwa kuvuna viingilio.

Ukuta wa Simba

Safu ya ulinzi ya Simba imeendelea kuonyesha ubora ikicheza mechi ya tatu mfululizo kwenye ligi bila kuruhusu bao huku kipa wake Camara akiendelea kuwaacha makipa wengine katika vita ya clean sheet akiwa nazo 11 akiwaacha Djigui Diara wa Yanga na Patrick Munthali wenye nane kila mmoja