Simba yaichapa TMA, yafuzu 16 bora

SIMBA imetinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TMA Stars kwenye mchezo uliochezwa  Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, leo, ambapo sasa inakwenda kucheza dhidi ya Big Man.

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba ilionekana kutawala huku ikisukuma mashambulizi kupitia maeneo ya pembeni ambayo walicheza Valentine Nouma, Shomari Kapombe, Ladack Chasambi na Joshua Mutale.

Katika dakika 10 za kwanza, TMA ilionekana kuiheshimu Simba muda mwingi ikibaki eneo lake kabla ya kuamua kufunguka na kuruhusu mabao mawili ya haraka katika dakika ya 16 na 19.

Bao la kwanza la Simba lilifungwa kwa ustadi na Nouma kwa faulo, kisha la pili likitokana na krosi ya Chasambi iliyomfanya nyota wa TMA, Sixtus Sabilo kujifunga akiwa kwenye harakati za kuokoa.

Hata hivyo Simba ilikuwa na nafasi ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mengi zaidi lakini ilipoteza nafasi kadhaa za wazi hasa kuanzia dakika ya 20 hadi 35 kupitia Leonel Ateba.

Licha ya mabadiliko kadhaa ambayo Simba ilionekana kuyafanya katika kipindi cha pili ikiwemo kuingia kwa Omary Omary aliyechukua nafasi ya Augustine Okejepha, bado ilionekana kushindwa kutumia vizuri nafasi ilizotengeneza.

Miongoni mwa nafasi hizo ni ile ya Ateba baada ya pasi ya Edwin Balua aliyeingia kipindi cha pili kabla ya mshambuliaji huyo kufunga bao la tatu na la mwisho kwenye mchezo huo.

KAGOMA AGEUZWA BEKI

Baada ya Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0, Fadlu aliamua kumpumzisha beki wake wa kati Abdulrazak Hamza na nafasi yake kuingia kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma.

Wakati ikisubiriwa kuona nini kitatokea mwanzoni mwa kipindi cha pili, Kagoma akaonekana kushuka eneo la chini na kucheza sambamba na Chamou Karaboue.

Licha ya kwamba haijazoeleka kuona Kagoma akicheza eneo hilo, lakini alimudu vizuri katika dakika 45 za kipindi cha pili huku akionyesha usahihi wake wa maamuzi katika upigaji wa pasi.

TMA ILIZIDIWA HAPA

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao walikuwa wakikaba katika nusu yao, TMA ilioenkana ikifanya makosa kwa wachezaji wake kuacha mianya ambayo wachezaji wa Simba walikuwa wakiitumia.

Mabeki wa TMA wakiongozwa na Asanga na Vedastus walipata tabu kwa Ateba, huku wakiacha nafasi kwa washambuliaji wengine, Chasambi, Mutale na Awesu Awesu ambao walikuwa wakibadilisha nafasi.

Hilo lilionekana kuwapa tabu kiasi cha muda mwingi kuonekana kukaribisha mashambulizi ya Simba, miongoni mwa nyota wao ambao walionekana kuwa na uhai katika eneo lao la mbele ni pamoja na Sabilo.

FADLU AFUMUA KIKOSI

Tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wa mwisho wa wekundu hao wa Msimbazi dhidi ya Coastal Union kwenye ligi, kocha wa Simba, Fadlu Davids aliamua kufanya mabadiliko ya wachezaji sita.

Mabadiliko hayo kwenye kikosi chake cha kwanza cha wachezaji 11, yalikuwa katika eneo la beki wa kulia ambapo alirejea kikosini Shomary Kapombe badala ya David Kameta ‘Duchu’ huku eneo la kiungo cha kati akipata nafasi Augustine Okejepha badala ya Yusuph Kagoma.

Pembeni katika kushambulia walianza Ladack Chasambi na Joshua Mutale badala ya Elie Mpanzu na Kibu Denis, nyuma ya mshambuliaji wa mwisho alianza Awesu Awesu badala ya Jean Charles Ahoua.

Huku mshambuliaji wa mwisho akiwa na Leonel Ateba badala ya Steven Mukwala ambaye alipachika mabao matatu kule Arusha dhidi ya Coastal Union.

KILUVYA UNITED 0-3 PAMBA JIJI

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Pamba Jiji waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kiluvya United.

Mabao ya Pamba yamefungwa na Christopher Oruchum, Ally Ramadha Oviedo na Yonta Camara. Ushindi huo unaifanya kufuzu hatua ya 16 Bora na kwenda kukutana na Mashujaa.

Timu 14 zimefuzu hatua ya 16 bora kabla ya jana jioni Kagera Sugar kucheza dhidi ya Namungo huku leo Yanga ikiikaribisha Coastal Union. Timu hizo ni Singida Black Stars, KMC, Mbeya City, Mtibwa Sugar, JKT Tanzania, Mbeya Kwanza, Mashujaa, Pamba Jiji, Stand United, Giraffe Academy, Simba, Big Man, Tabora Utd na Songea FC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *