Simba yahamishia hesabu CAF

Mastaa wa Simba kuanzia jana walianza mapumziko ya siku tatu wakati mashabiki wao wakifurahia ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya KMC lakini kocha wao Fadlu Davids amesema sasa anahamishia hesabu zake kwenye michuano ya CAF.

Simba ipo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mchezo wake wa kwanza itavaana na Bravos do Maquis FC ya Angola Novemba 27, kwenye Uwanja wa Mkapa, ukiwa ni mchezo wao wa mashindano unaofuata.

Simba imekuwa na matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo 10 imeshinda nane na kutoka sare mchezo mmoja huku ikifunga mabao 21 na kuruhusu matatu tu kwenye michezo hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Fadlu amesema ni jambo jema kupata mapumziko marefu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wakati wachezaji wengine wakiwa kwenye michuano ya kutafuta kufuzu Afcon 2025.

Fadlu ambaye timu yake ilitakiwa kucheza na Pamba Novemba 21, lakini mchezo huo umeahirishwa, alisema muda huo watautumia vizuri kujipanga sawasawa dhidi ya Bravos Maquis kwa kutafuta kila taarifa za ubora wao.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema mapumziko hayo pia yatawasaidia wachezaji wake kujiandaa kwa utulivu huku pia mastaa wake watakaokwenda timu za taifa kupata muda mzuri wa kurejea na wao kujiandaa wakiwa kama timu.

“Tulilazimika kufanya mzunguko wa wachezaji ili kila mmoja apate muda wa kupumzika sawasawa, ratiba ilikuwa ngumu sana lakini nimeona kuna mechi imeondolewa ya ligi hii itatupa nafasi nzuri kujiandaa na mechi ya kwanza ya makundi, nipongeze sana,” alisema Fadlu.

“Akili yetu sasa itajikita huko kwenye shirikisho, kwetu sisi makocha tutakuwa na muda wa kujua kila taarifa za wapinzani wetu juu ya ubora wao lakini huku tukiendelea na maandalizi taratibu.

Aidha Fadlu aliongeza kuwa katika maandalizi yao hayo watahakikisha wanaongeza kasi ya kutumia nafasi kwani mechi hizo za CAF hazizalishi nafasi nyingi za kufunga.

“Tunatakiwa kuanza vizuri, ikiwezekana kwa ushindi mkubwa na bila kuruhusu bao, kitu muhimu hapa ni sisi kutumia nafasi tutakazotengeneza kwa wingi hizi ni mechi ambazo hazina nafasi nyingi.

“Angalia mechi iliyopita (dhidi ya KMC) sawa, tulishinda vizuri lakini kipindi cha kwanza tulistahili kupata mabao hata matatu lakini hatukuwa kwenye utulivu mkubwa hili ni lazima tulifanyie kazi ndani ya huu muda.”

Mbali na Simba, mechi ya Yanga ya Ligi Kuu iliyokuwa inafuata ni dhidi ya Fountain Gate nayo imesogezwa mbele ili kuwapa nafasi nzuri ya kujiandaa na mchezo wa hatua ya Makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Mechi hii ya Yanga inatarajiwa kupigwa Novemba 26 kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.