Simba yaendeleza ubabe Ligi Kuu

Simba imeendeleza ubabe katika mechi za ugenini za Ligi Kuu msimu huu huku ikizidi kujichimbia kileleni mwa msimamo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jana.

Ushindi huo ni wa tano mfululizo kwa Simba ugenini katika Ligi Kuu baada ya kuzichapa Azam FC, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons na Mashujaa na sasa imefikisha pointi 28 ambazo zinaifanya iendelee kutamba kileleni.

Lionel Ateba liifungia Simba, bao la ushindi katika mechi ya jana kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 23 akimaliza ukame wa kucheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu ambazo alicheza bila kufumania nyavu tangu alipofanya hivyo dhidi ya Azam FC, Septemba 29.

Penalti hiyo iliamriwa na refa Hussein Katanga baada ya Ateba kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari na beki wa Pamba, Christopher Oruchum.

Haikuwa ni mechi ambayo ilitoa fursa kwa wachezaji wa timu zote mbili kuonyesha ufundi kutokana na hali ya eneo la kuchezea la Uwanja wa CCM Kirumba kuonekana kuwa ya unyevu pengine kutokana na mvua zilizonyesha jijini Mwanza kuanzia juzi, jambo lililozilazimisha timu hizo kupiga pasi ndefu mara kwa mara.

Mara baada ya filimbi ya kuashiria muda wa mapumziko kupulizwa, wachezaji wa Pamba Jiji FC walionekana kumzonga refa Hussein Katanga katika kile kinachoweza kutafsirika kuwa ni kutoridhishwa na uamuzi wake wa kutomuonyesha kadi nyekundu Shomari Kapombe baada ya kumfanyia madhambi George Mpole ambaye alikuwa akielekea langoni mwa Simba.

Hata hivyo, pembeni ya Kapombe kulikuwa na beki Chamou Karaboue wakati faulo hiyo inafanyika jambo ambalo pengine lilimfanya refa Katanga kutafsiri kuwa Kapombe hakuzuia nafasi ya wazi ya kufunga bao ya Pamba Jiji FC.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko ambapo Pamba ilimtoa Paulin Kasindi na kumuingiza Alain Mukeya na Simba ilimpumzisha Charles Ahoua ambaye nafasi yake ilichukuliwa na Kibu Denis.

Dakika 13 baadaye, Simba iliwatoa Awesu Awesu na Debora Mavambo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Augustine Okejepha na Omary Omary.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na faida zaidi kwa Pamba kwani ilionekana kutawala mchezo kwa muda mwingi wa kipindi na kulishambulia mara kwa mara lango la Simba lakini ilikosa umakini wa kutumia baadhi ya nafasi ambazo ilipata.

Miongoni mwa nafasi hizo ni ile iliyookolewa kwa ustadi na kipa Moussa Camara katika dakika ya 60 iliyotokana na shuti la James Mwashinga na kuwa kona ambayo Justin Omary aliunganisha kwa kichwa kilichopaa juu ya lango.

Dakika ya 81, Pamba walipata nafasi nzuri nyingine ya kusawazisha bao kupitia Samuel Antwi ambaye alipokea pasi nzuri ya Eric Okutu akiwa analitazama lango la Simba na kupiha shuti lililodakwa na kipa Camara.

Uimara wa safu ya ulinzi ya Simba uliiwezesha timu hiyo kumaliza salama dakika 90 bila kuruhusu bao na hivyo kumfanya kipa Camara kufikisha mechi ya nane msimu huu kucheza bila nyavu zake kutikiswa kwenye Ligi Kuu.

Hadi refa Katanga anapuliza filimbi ya mwisho, Simba ilifanikiwa kulinda ushindi wake na kuvuna pointi tatu muhimu.
Kwenye mechi ya jana, Pamba ilifanya pia mabadiliko ya kuwatoa Saleh Masoud, Daniel Joram na Samuel Antwi ambao nafasi zao zilichukuliwa na Kelvin Nyanguge, Eric Okutu na Freddy Selemani.

Simba iliwatoa pua Ladack Chasambi na Lionel Ateba ambao nafasi zao zilichukuliwa na Steven Mukwala na Abdulrazack Hamza.

Wachezaji 11 walioanza katika kikosi cha Pamba ni Yona Amosi, Christopher Oruchumu, Ibrahim Abdallah, Justine Omary, Salehe Masoud, Paulin Kasindi, George Mpole, Samuel Antwi, James Mwashinga, Mwaita Gereza na Daniel Joram.

Kikosi cha Simba kilianza na Moussa Camara, Shomari Kapombe, Valentine Nouma, Chamou Karaboue, Che Malone, Fabrice Ngoma, Ladack Chasambi, Charles Ahoua, Lionel Ateba, Debora Mavambo na Awesu Awesu.