Simba yaenda makundi kibabe

Kama kawaida. Ndivyo baadhi ya mashabiki waliojazana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati Simba ikiing’oa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa mabao 3-1 na kutinga kibabe makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika walivyokuwa wakitamba.

Mastaa walioifungia Simba kwenye mechi hii walikuwa ni Kibu Denis, Lionel Ateba na Edwin Balua waliotupia mabao hayo yaliyoiangamiza Al Ahli Tripoli mbele ya kocha wa timu ya taifa ya Libya, Milutin Sredojevic ‘Micho’ anayedaiwa kukodiwa kwa muda na timu hiyo akiwa jukwaani.

Kibu na Ateba walianza pamoja kikosini jana na ushirikiano wao na nyota wengine walioanza kikosi cha kwanza waliizima kabisa Al Ahli na kuifanya Simba itinge makundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1, kwani mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Tripoli wiki iliyopita ulimalizika kwa suluhu.

Simba sasa inakuwa imetinga makundi kwa mara sita ndani ya misimu saba ya michuano yote ya CAF ngazi ya klabu, lakini ikiwa ni mara ya pili katika michuano hiyo ya Shirikisho baada ya ile ya msimu wa 2021-2022, ilipokwamia robo fainali.

Katika mchezo wa jana uliohudhuriwa na mashabiki wengi wa Msimbazi, Simba iliupiga mpira mwingi na kuonyesha wazi ilikuwa na dhamira ya kuifuata Yanga iliyotanguliza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika juzi kwa kuing’oa CBE ya Ethiopia na kuifanya kwa misimu mitatu mfululizo Tanzania kuingiza timu mbili.

Mechi ilivyokuwa

Simba ililazimika kutoka nyuma na kutengeneza ushindi huo baada ya Ahli kutangulia kupata bao dakika ya 17 mfungaji akiwa straika kutoka Angola, Cristivao Paciencia ‘Mabululu’  aliyefunga kirahisi baada ya mabeki wawili wa Simba Fondoh Che Malone na Abdulrazack Hamza ambaye aliiumia baadaye na kutoka kushindwa kuokoa mpira.

Shambulizi hilo lilitokana na mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na nahodha wa timu hiyo, Hamdou Houni kisha beki Ahmed Elrtbi kutengeneza krosi safi ya kichwa iliyokwenda kuwachanganya mabeki wa Simba na mpira kumkuta Mabululu.

Hata hivyo, Simba ilisawazisha bao dakika ya 36 kwa shambulizi la adhabu, likiwekwa kimiani na Kibu Denis aliyepiga tik tak, akipokea mpira wa kichwa toka kwa Che Malone.

Sekunde chache kabla ya mapumziko Simba iliongeza bao la pili kupitia kwa Lionel Ateba akipokea pasi ya kiungo wa Ahli, Mourad Hedhli aliyekuwa akirejesha mpira nyuma, kisha mshambuliaji huyo kwenda kufunga kirahisi na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, hata hivyo wakati mashabiki wakiwa na presha, Edwin Balua aliifungia Simba bao safi la tatu katika dakika ya 90 ya mchezo.

Camara Kibu, ateba acha tu

Kama kuna mchezaji wa Simba aliiweka Al Ahli katika wakati mgumu basi wa kwanza ni Kibu ambaye alionyesha kiwango cha juu sana kwenye mechi hii.

Kibu alikuwa wa moto akiwambiza mabeki wa Ahli, hasa kipindi cha pili na kuwapa nguvu Simba ikisaka mabao zaidi, pia kuna Ateba alikuwa mwiba kwa Walibya akitengeneza mashambulizi makali lakini sifa za mechi hiyo ziende kwa kipa wa Simba Moussa Camara ambaye aliokoa michomo mikali kwenye mechi hii.

BAO LA ATEBA

Waamuzi wa mchezo huo, dakika ya 64 waliinyima Simba bao lililoonekana halali kabisa lililowekwa kimiani tena na Ateba, aliyepokea pasi safi na Ahoua, lakini wakati akishangilia na wenzake, mwamuzi wa pili msaidizi Yamousa Syla kutoka Guinea alikuwa ameshaonyesha kibendera kuwa kuna mchezaji ameotea.

Mpanzu alikuwepo

Mapema Simba ilimshuhudia winga wao mpya, Elie Mpanzu akiwa jukwaani alipofika uwanjani hapo akiwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya wekundu hao Salim Mhene ‘Try Again’.

Mpanzu alikuwa amevalia fulana nyekundu ya Simba ikiandikwa jina lake Mpanzu nyuma na miwani meusi.

Kuungana na vigogo

Kitendo cha Simba kutinga makundi imeifanya sasa kuungana na vigogo wengine kwenye michuano hiyo wakiwamo watetezi, Zamalek ya Misri, RS Berkane ya Morocco, CS Sfaxien ya Tunisia, CS Constantine ya Algeria, sambamba na Stade Malien ya Mali na Luanda Sul ya Angola ambazo hadi jana jioni zilikuwa zimeshafuzu huku zikisubiri droo ya makundi Oktoba 7.

fedha ya kutosha

Kutinga makundi kumeihakikisha Simba kubeba Dola 400,000 (zaidi ya Sh 1 Bilioni), lakini ilivuna Sh 15 milioni za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya Goli la Mama’ kutokana na mabao matatu iliyofunga ambao kila bao thamani yake ni Sh 5 milioni.