Simba yaanza mambo, Fadlu akitaka usiri

KIKOSI cha Simba kimefanya mazoezi ya kwanza nchini Morocco baada ya kuwasili jana Alhamisi asubuhi.

Mazoezi hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Mazgan katika mji wa Jadida.

Wachezaji wote waliosafiri katika msafara wa Simba kuja Morocco wameshiriki katika mazoezi hayo.

Kabla ya mazoezi hayo kufanyika, kocha Fadlu Davids alitoa agizo la kuzuia waandishi wa habari na watu wengine ambao wamekuja na timu hiyo hapa kutazama mazoezi hayo.

Ni viongozi wachache sana ambao waliruhusiwa kushiriki katika mazoezi hayo ambayo yalianza kwa kunyoosha misuli na baadaye yakahamia katika mbinu.

Fadlu anaamini kitendo cha idadi kubwa ya watu kuhudhuria mazoezi kinaweza kuathiri program zake na mbinu kuelekea mechi hiyo dhidi ya RS Berkane.

Mazoezi hayo yalianza saa 11 jioni kwa saa za Morocco sawa na saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania.

Simba inajiandaa kuikabili RS Berkane Jumamosi ya Mei 17 ikiwa ni mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa mjini Berkane kabla ya kurudiana wiki moja baadae jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa Simba imejichimbia jijini Casablanca.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *