
Dar es Salaam. Simba ina kibarua kigumu dhidi ya Al Masry ya Misri kesho Jumatano, Aprili 09, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo inatakiwa kuibuka na ushindi wa tofauti ya mabao matatu ili iweze kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 2-0.
Wakati ikijiandaa na mchezo huo, takwimu za mchezo wa kwanza ugenini za zile za Ligi Kuu zinaonekana kutokuwa upande wa mshambuliaji chaguo la kwanza la timu hiyo, Lionel Ateba kulinganisha na mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Steven Mukwala.
Katika mchezo uliopita, Ateba alionekana kupoteza nafasi nyingi ambazo alipata ndani ya eneo la hatari na haikushangaza kuona mtandao unaojishughulisha na utoaji na utunzaji wa takwimu za soka wa www.fotmob.com ukimuweka mshambuliaji huyo kutoka Cameroon katika nafasi ya pili kwenye kundi la wachezaji waliofanya vibaya zaidi katika mechi hiyo kwa kumpa alama 5.7 kati ya 10 huku kipa wa Simba, Mousa Camara akitajwa kuwa ndiye aliyefanya vibaya zaidi ambapo alipewa alama 4.3.
Kwenye Ligi Kuu nako, Ateba katika mechi 17 alizocheza amefanikiwa kufunga mabao nane akitoa pasi tatu za mabao akitumia dakika 1,176.
Mukwala naye ndani ya mechi 20 alizocheza akiwa ameanza kwenye michezo michache, amefunga mabao tisa akiwa na pasi mbili za mwisho akitumia dakika 736 pekee kutengeneza namba hizo.
Kuelekea mchezo dhidi ya Al Masry kesho, nyota wa zamani wa Simba wamelishauri benchi la ufundi la timu hiyo kufikiria kumpa nafasi ya kutosha Mukwala lakini kama litaamua kufanya hivyo kwa Ateba, basi mshambuliaji huyo anatakiwa kuhakikisha anafunga mabao ili asiiweke timu katika wakati mgumu na kuangusha imani ya kocha kwake.
“Kwanza lazima tukubaliane mwenye maamuzi ya mwisho ya nani acheze ni kocha. Nadhani tumuachie yeye afanye maamuzi yake, kocha ndiye anayeona wachezaji wake kuanzia mazoezini.
“Inawezekana kocha anataka kumtumia Ateba lakini ninachoweza kumshauri azungumze na wasaidizi wake kwenye timu kama watamwambia aanze na Mukwala badala ya Ateba basi ajaribu kuwasikiliza kwa kuwa watakuwa na kitu wameona kupitia wachezaji hao wawili.
“Kwangu mimi naamini Simba bado ina nafasi ya kufanya mambo mazuri kwa kutengeneza ushindi mzuri kitu muhimu wachezaji wajitambue na kufanyiana wepesi ili wapate matokeo mazuri wanayoyataka,”amesema gwiji wa timu hiyo Abdallah Kibadeni.
Kwa upande wa kiungo wa zamani, Dua Said amesema ingawa kocha Fadlu ameyaona mapungufu ya kikosi chake kilivyocheza mchezo wa kwanza lakini amewataka wachezaji wanaocheza safu ya mbele kuanzia viungo kucheza kwa muunganiko kumpa urahisi mshambulijiaji huyo.
“Kocha atakuwa ameona namna makosa waliyoyafanya kwenye mechi ya kwanza. Mimi naona Simba ina nafasi ya kutengeneza matokeo mazuri katika mechi. Kati ya Waarabu ambao nimewahi kuwaona, hawa Al Masry, Simba inatakiwa kumalizana nao kwa kuwa wapo kwenye uwezo wao,”amesema Dua.
Dua ameongeza, “kuhusu hao washambuliaji, ukitazama namna Atena alivyocheza mchezo wa kwanza hata ukiniuliza mimi nitakwambia ni bora aanze Mukwala lakini shida yangu ni tofauti kidogo.
“Inawezekana tunamuona Ateba tatizo lakini tuwaangalie wale viungo wanaocheza kumzunguka, Ahoua (Jean Charles) na kina Mpanzu (Elie) na Kibu (Denis) ukiona namna wanavyocheza wanampa wakati mgumu Ateba wanamuacha mbali sana lakini pia waache ubinafsi.”