
Kuna saa 24 za moto kwa Simba na Yanga kujiuliza wanaziendeaje mechi zao zilizoshikilia maana kubwa katika kufikia malengo yao msimu huu. Saa hizo zinaanzia leo katika maandalizi ya mwisho kabla ya kesho Jumatano kushuka dimbani kila mmoja na hesabu zake. Lakini kabla kesho haijafika, leo kuna mechi za kuamua jambo barani Ulaya.
Ligi Kuu England ambayo ilisimama tangu Machi 16 mwaka huu kupisha kalenda ya FIFA, inarejea leo kwa kupigwa mechi tatu. Saa 3:45 usiku ni London Dabi kati ya Arsenal dhidi ya Fulham, kisha Wolves itaikaribisha West Ham huku saa 4:00 usiku ikiwa zamu ya Nottingham Forest kupambana na Manchester United.
Kule Italia kuna mechi ya nusu fainali ya Coppa Italia, Empoli dhidi ya Bologna saa 4:00, kabla ya hapo, itaanza nusu fainali nyingine ya DFB Cup nchini Ujerumani kati ya Arminia Bielefeld na Bayer Leverkusen saa 3:45 usiku. Pia Hispania kuna mchezo wa nusu fainali ya Copa del Rey, Real Madrid itacheza dhidi ya Real Sociedad kuanzia saa 4:30 usiku.
Tukirudi kwa timu zetu za nyumbani, Simba ipo Misri kukabiliana na Al Mary ukiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi utakaoanza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Suez.
Kwa upande wa Yanga, watakuwa zao Tabora kukabiliana na Tabora United kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikichezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kuanzia saa 10:00 jioni.
SIMBA VS AL MASRY
Kikosi cha Simba kipo Misri tangu Ijumaa iliyopita kikiweka kambi kwenye Mji wa Ismailia, yalipo makazi ya wapinzani wa Al Masri, Klabu ya Ismailia.
Uamuzi wa Simba kujificha huko ni kuhitaji utulivu zaidi kwani unaambiwa sehemu waliyopo hakuna nafasi kwa Al Masry kujipenyeza kutokana na kuwa wapinzani wakubwa wa Ismailia.
Hata hivyo, Simba inakabiliwa na mchezo mgumu wa ugenini huku rekodi zikionekana kuwakataa baada ya kufeli kufuzu hatua ya nusu fainali katika mara sita walizocheza robo fainali michuano ya CAF kuanzia 2018-2019.
Simba inaisaka rekodi mpya chini ya Kocha Fadlu Davids ambaye mwenyewe amekiri anakwenda kukutana na timu ngumu lakini anaamini wanaweza kufanya vizuri kufuatia kambi yao ya maandalizi ya msimu kuiweka huko Misri.
“Kukabiliana na Al Masry haitakuwa rahisi. Lakini tulikuwa na maandalizi ya msimu mpya nchini Misri na tunajua nini cha kutarajia tutakapocheza mkondo wa kwanza nchini Misri,” alieleza Fadlu.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema kikosi chake kipo tayari kukabiliana na Al Masry kwani masuala ya ufundi yapo vizuri kutokana na kuangalia mechi za wapinzani wao hao na kufahamu mbinu gani nzuri za kukabiliana nao.
“Tupo tayari kuwakabili hasa eneo la kiufundi. Tayari tumeziangalia mechi za Al Masry na kujua vitu vya kitaalam na mpango gani wa mchezo tunaokwenda kucheza kwa kuweka mkakati wa kusaka ushindi dhidi yao,” alisema Fadlu.
Rekodi zinaonesha Simba wakati inashindwa kufuzu nusu fainali katika mashindano ya CAF kuanzia 2018-2019 walipocheza robo fainali tano kabla ya hii kuwa ya sita, ilishindwa kufanya vizuri zaidi ugenini.
Matokeo ya mechi za kwanza wakati ikipambania kufuzu nusu fainali, Simba mara mbili imeshinda na zote nyumbani huku moja ikiwa suluhu na mbili ikipoteza.
Mechi ambazo Simba ilionekana inakwenda kufanya maajabu katika marudiano ni ile ya kwanza ilipotoka 0-0 nyumbani dhidi ya TP Mazembe (2018-2019) lakini ikaenda ugenini ikachapwa 4-1.
Kisha msimu wa 2021–22 nyumbani iliifunga Orlando Pirates bao 1-0, ugenini ikaruhusu kufungwa 1-0 na kupoteza kwa penalti 4-3.
Pia msimu wa 2022–2023 iliichapa Wydad bao 1-0 nyumbani, ugenini ikafungwa kwa idadi hiyo ya mabao na kuondoshwa kwa penalti 4-3.
Hata hivyo, msimu wa 2020–2021, Simba ilianzia ugenini nchini Afrika Kusini na kufungwa 4-0, ilionekana kuwa na mlima mrefu wa kuupanda na mechi ya marudiano nyumbani ikashinda 3-0 na kushindwa kufuzu baada ya matokeo ya jumla kuwa 4-3.
Al Masry ina kumbukumbu ya kucheza na Simba michuano hii msimu wa 2017-2018 katika hatua ya kwanza na mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilimalizika kwa sare ya 2-2, kisha marudiano iliyochezwa Misri ikawa 0-0, Simba ikatolewa kwa kanuni ya mabao ya ugenini.
TABORA VS YANGA
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara kesho wanakwenda kujiuliza kwa Tabora United, timu ambayo duru la kwanza iliwafanya kitu kibaya kwa kufungwa nyumbani 3-1 wakati kocha akiwa Miguel Gamondi ambaye baada ya kipigo hicho akaondolewa.
Tabora United ambayo inaendelea kupambana kutotoka nafasi za juu kufuatia kuwa ya tano na pointi 37, imekuwa haina matokeo mazuri kwenye uwanja wake wa nyumbani huku Yanga ikipania kufanya kweli ikinolewa na kocha mwingine, Miloud Hamid.
Yanga na Tabora zinakutana zote zikiwa na makocha tofauti na wale waliokuwepo mechi ya kwanza kwani hivi sasa Tabora inafundishwa na Mzimbabwe Genesis Mang’ombe aliyechukua nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi Makiadi.
Hamdi anakwenda kukutana na Tabora akiwa na rekodi ya kuiongoza Yanga kucheza mechi tano za ligi akishinda nne na sare moja huku timu yake ikifunga mabao 16 ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi.
Tabora iliyoruhusu mabao 28 katika mechi 23 za ligi msimu huu, ina kazi kubwa ya kufanya mbele ya Yanga kwani safu yake ya ulinzi imeonekana kuwa dhaifu ikiwa na wastani wa kuruhusu bao kila mechi.
Yanga inasaka pointi tatu zitakazowaweka zaidi kileleni kwa kufikisha 61, huku Tabora nayo inasaka pointi tatu ifikishe 40, ikiifukuzia Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne na pointi 44.