
Unakumbuka mwaka 1993 wakati Simba inacheza fainali ya Kombe la CAF ambalo baadaye 2004 likaunganishwa na Kombe la Washindi kisha kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika? Basi kwa kukukumbusha tu ni kwamba kabla ya mechi ya nusu fainali dhidi ya Atlético Sport Aviação, hali ilikuwa kama hivi ambavyo Jumapili hii Simba wanakwenda kucheza dhidi ya Stellenbosch.
Kipindi hicho Simba hatua ya robo fainali iliwaondosha Waarabu, USM El Harrach ya Algeria, ikishinda nyumbani 3-0 na kupoteza ugenini 2-0, ikavuka kwa matokeo ya 3-2. Kuna mfanano kidogo na ilivyokuwa msimu huu kwani robo fainali pia Simba imewaondosha Waarabu lakini safari hii wanaotokea Misri. Mechi ya ugenini Simba ilifungwa 2-0, ikaja kushinda nyumbani 2-0, matokeo ya jumla yakawa 2-2, mikwaju ya penalti ikawavusha Simba kwa matokeo ya 4-1. Yale ya mwaka 1993, yanaweza kutokea kwa Simba mbele ya Stellenbosch. Ipo hivi; Mwaka 1993, mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CAF, Simba ilianzia nyumbani dhidi ya Atletico Sport Aviacao kutoka Angola, ikashinda 3–1, kisha ikaenda ugenini kupata matokeo ya 0-0, ikatinga fainali.
Miaka 32 mbele kwa maana ya msimu huu, Simba nusu fainali inaikaribisha Stellebosch katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni.
Ni mchezo ambao Simba ili kusafisha njia ya kucheza fainali, inapaswa kupata ushindi mzuri kabla ya marudiano Aprili 27 nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, mchezo huu umekaa kimtego huku kila upande ukiwa na hesabu zake. Hilo linafanya mchezo wenyewe kuwa na hatari kubwa ya kutokea matokeo ya kushangaza.
WALIOISHIKA MECHI
Katika mechi nane ambazo Simba imecheza kuanzia hatua ya makundi hadi robo fainali, kipa Moussa Camara, mawinga Kibu Denis na Elie Mpenzu pamoja na kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua ndio wamechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha timu hiyo nusu fainali na wanaweza kuibeba zaidi ikiwa watalinda au wataongeza ubora wao uwanjani dhidi ya Stellenbosch. Camara, aliokoa mikwaju miwili ya penalti katika mechi ya marudiano ya robo fainali dhidi ya Al Masry lakini kabla ya hapo aliokoa penalti moja katika muda wa kawaida kwenye mechi ya makundi dhidi ya Onze Bravos ya Angola.
Hajaishia hapo kwa Camara kuokoa penalti tu, kwani katika mechi hizo nane zilizopita za Simba kwenye mashi-ndano hayo ameokoa michomo 16 ikiwa ni wastani wa hatari mbili kwa mchezo na haishangazi kuona akishika nafasi ya tatu katika orodha ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao (clean sheet) akifanya hivyo katika michezo minne. Licha ya kuichezea Simba mechi tano tu kwenye mashindano hayo kwa vile alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili, winga Elie Mpanzu amekuwa na matokeo chanya kwa Simba ndani ya muda mfupi alioitumikia.
Mpanzu ameshahusika na mabao mawili katika mechi hizo tano alizoichezea Simba, akifunga moja na kupiga pasi moja ya mwisho, lakini anashika nafasi ya pili katika chati ya wachezaji waliokokota mpira kwa ukamilifu kwenye mashindano hayo, akiwa na wastani wa kufanya hivyo mara 3.6 kwa mechi.
Kibu ndiye kinara wa Simba kwa ufungaji kuanzia hatua ya makundi akifunga mabao matatu lakini pia ndiye anayeongoza katika timu hiyo kwa kuwa na wastani mzuri wa kupiga mashuti yanayolenga lango kwa usahihi ambapo kwa mchezo ana wastani wa shuti 1.3.
Takwimu zinaonyesha kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho ndani ya Simba akifanya hivyo mara mbili huku akishika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo kiujumla na amefunga mabao mawili.
Katika utengenezaji wa nafasi Ahoua ndiye mchezaji hatari zaidi wa Simba kwani amefanya hivyo mara 19, akishika nafasi ya pili katika chati ya mashindano hayo na katika nafasi hizo 19, nafasi za hatari zaidi ni nne.
Pia uwepo wa Abdulrazak Hamza unaifanya Simba kuwa salama eneo la beki ya kati ambalo kwa sasa anacheza sambamba na Chamou Karaboue, pembeni tunaweza kuendelea kuwaona Shomary Kapombe na Mohammed Hussein.
Kwa Stellenbosch, Sage Stephens atakuwa golini, huku Andre de Jong akipewa majukumu ya kuongoza safu ya ushambuliaji huku kukosekana kwa Ashley Cupido, ni wazi majukumu yote ya kuisumbua safu ya ulinzi ya Simba yatakuwa kwake.
Mshambuliaji huyo raia wa New Zealand, ana mabao mawili kwenye michuano hii, hivyo ni mchezaji wao tegemeo.
KIBURI CHA WASAUZI
Kwa upande mwingine, Stellenbosch ambao ni wageni katika michuano ya CAF wanakuja na morali ya kumtoa bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Zamalek.
Kocha wao Steve Barker, akiwa na timu yake, anajivunia mafanikio waliyopata katika safari yao ya kufika nusu fainali ya CAF. Timu hii, licha ya kuwa na wachezaji wachache wenye uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa, imeonyesha sifa za kupambana na timu kubwa barani Afrika.
Barker ameongeza kuwa Sage Stephens, nahodha wa timu hiyo na mlinda lango, atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka uwanjani, baada ya kurejea kutoka majeruhi.
“Sisi ni timu yenye roho ya kupambana. Tumefanya maandalizi yetu vizuri na tunategemea kufanya vizuri dhidi ya timu kubwa kama Simba. Tunajua ni mchezo wa kihistoria, lakini tunajivunia safari yetu na tutapambana kwa nguvu zote,” alisema Barker.
Kiburi hicho cha Wasauzi, kinaweza kuwafanya Simba kuingia kwa tahadhari kubwa sana kukabiliana nao.
HISTORIA NA REKODI
Simba ina historia ndefu ya kushindana na timu za Afrika Kusini kwenye michuano ya CAF na hii itakuwa mara ya nne kukutana na timu kutoka taifa hilo huku ikiwa na rekodi nzuri inapocheza uwanja wa nyumbani kwani haijawahi kupoteza ikishinda mara zote tatu zilizopita.
Mbali na kuwa na rekodi nzuri ya kushinda nyumbani, lakini Simba imeiondosha mara moja tu timu ya Sauzi katika mtoano huku nyingine ikishindwa kupenya. Hiyo inaifanya Simba kuwa na mtihani mzito mbele ya Stellenbosch kwani licha ya rekodi yao nzuri ya nyumbani kuwabeba, lakini inahukumiwa na rekodi ya jumla kwa kuvuka hatua inayofuata. Katika mara tatu Simba ilipocheza nyumbani dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini, ilishinda kwa penalti 9-8 dhidi ya Santos kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003. Mikwaju hiyo ya penalti iliivusha Simba ambayo ilikwenda kukutana na Zamalek na kuiondosha pia, kisha ikafuzu makundi. Katika michezo miwili ya mtoano dhidi ya Santos, ilianzia ugenini Aprili 13, 2003 matokeo yakiwa 0-0 kisha marudiano nyumbani ikawa 0-0, ndipo penalti zikaivusha Simba. Mwaka 2021, Simba walicheza dhidi ya Kaizer Chiefs hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Baada ya kupoteza kwa 4-0 ugenini, walijitahidi kurejesha matumaini kwa kushinda 3-0 nyumbani, lakini hawakufanikiwa kutinga hatua inayofuata kutokana na matokeo ya jumla kuwa 4-3. Katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 2022, walikutana na Orlando Pirates, ambapo baada ya kushinda 1-0 nyumbani, walishindwa kufuzu baada ya kufungwa 1-0 ugenini, na hatimaye kupoteza kwa penalti 4-3. Rekodi hii inawafanya Simba kukumbuka yaliyotokea mechi mbili za mwisho dhidi ya Wasauzi ili kutorudia makosa ya kushindwa kuvuka hatua inayofuata. Hata hivyo, Simba ina matumaini makubwa kwa mchezo huu dhidi ya Stellenbosch, ikiwa na nyota kama Steven Mukwala mwenye mabao tisa kwenye ligi na moja kimataifa, Jean Charles Ahoua mwenye mabao 12 katika ligi na mawili kimataifa, Kibu Denis mwenye mabao matatu CAF na Elie Mapanzu mwenye bao moja, ambao ni wachezaji muhimu katika kikosi cha Fadlu Davids. Pia Simba katika mechi za Kombe la Shirikisho msimu huu, imeshinda mechi zote tano za nyumbani, hivyo hadi sasa ina asilimia 100 za ushindi kulinganisha na Stellenbosch ambayo haipo vizuri ugenini kwani imepoteza mbili na sare moja, ikishinda tatu kati ya mechi sita. Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Simba haina rekodi mbaya, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC mchezo wa mwisho kucheza hapo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Septemba 26, 2024. Hata hivyo, Simba licha ya kuwa huo utakuwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimataifa kucheza uwanjani hapo, lakini ina uzoefu nao huku mechi kumi za mwisho ikiondoka na ushindi mara saba, ikipoteza mbili na sare moja. Matokeo ya mechi hizo kumi za mwisho ambazo Simba imecheza uwanjani hapo yapo hivi; Azam 0-2 Simba (Ligi Kuu), Simba 1-0 Azam (Fainali Muungano 2024), KVZ 0-2 Simba (Nusu fainali Muungano 2024), Mlandege 1-0 Simba (Fainali Mapinduzi 2024), Singida 1-1 (2-3penalti) Simba (Nusu fainali Mapinduzi 2024), Simba 1-0 Jamhuri (Mapinduzi 2024), Simba 0-0 APR (Mapinduzi 2024), JKU 1-3 Simba (Mapinduzi 2024), KVZ 0-1 Simba (Mapinduzi 2023) na Simba 0-1 Mlandege (Mapinduzi 2023).
MASTAA SIMBA WAFUNGUKA
Mastaa wa Simba wakiwemo Mpanzu, Ahoua, Hamza na Mukwala wamesema kuwa wako tayari kuonyesha kiwango cha juu katika mchezo.
“Tunaijua Stellenbosch ni timu bora na yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini sisi pia tuna wachezaji bora na tunajua tunachohitaji kufanikisha. Tutacheza kwa umakini na umoja ili kufuzu kwa fainali. Hii ni nafasi ya kipekee kwetu, na tunataka kuhakikisha tunatumia kila nafasi kutengeneza ushindi,” alisema Mpanzu.
Naye Ahoua alisema: “Maandalizi yetu yamekuwa bora, na tunahitaji kuonyesha uwezo wetu uwanjani. Kila mchezaji yupo tayari kufanya kazi kwa ajili ya timu. Kila mchezaji anajua umuhimu wa mechi hii.”
Hamza ambaye ni beki wa kati, alisema: “Tuna makosa machache ambayo tumejifunza kutoka kwa mechi zilizopita, na tunajua tunachohitaji kufanya ili kuepuka makosa hayo. Stellenbosch ni timu nzuri, lakini sisi pia tuna nguvu kubwa, na tunajua kama tutacheza kwa umoja huku tukifuata mpango wetu wa mchezo, tuna nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri.”