
Mchezo baina ya Simba na Dodoma Jiji uliokuwa uchezwe Februari 15, 2025 sasa utachezwa Machi 14, 2025 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Ajali ambayo timu ya Dodoma Jiji ilipata Februari 10, 2025 mkoani Lindi wakati ikiwa safarini kutokea huko baada ya kucheza na Namungo FC siku moja nyuma, iliilazimisha Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) kuuahirisha mchezo ambao ulikuwa unafuata kwa timu hiyo dhidi ya Simba ambao sasa utachezwa Ijumaa ya wiki ijayo.
“BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imeupangia tarehe mchezo namba 148 wa Ligi Kuu ya NBC kati ya klabu ya Simba ya Dar es Salaam na Dodoma Jiji ya mkoani Dodoma, uliokuwa umeondolewa kwenye ratiba ya Ligi baada ya klabu ya Dodoma Jiji kupata ajali ya gari walipokuwa wakisafiria kutoka mkoani Lindi.
“Mchezo tajwa hapo juu sasa utafanyika Machi 14, 2025 kuanzia saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa KMC Complex uliopo mkoani Dar es Salaam. Wadau wote wa mchezo huo, zikiwemo klabu shiriki, wamepewa taarifa hii kwa ajili ya kuendelea na taratibu za maandalizi.
“Bodi inawatakia wadau wote maandalizi mema ya mchezo huo pamoja na mingine inayofuata,” imefafanua taarifa ambayo imetolewa na TPLB leo.
Simba imekuwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Dodoma Jiji pindi inapokutana nayo ikiwa nyumbani lakini hata ugenini kwani imepata ushindi katika mechi zote tisa za Ligi Kuu ambazo imewahi kukutana na timu hiyo kutoka jijini Dodoma.
Katika mechi hizo tisa, Simba imefunga mabao 16 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.
Na Simba imekuwa miongoni mwa timu zinazotumia vyema uwanja wa nyumbani msimu huu nyuma ya Yanga na Azam ambazo ziko juu yake ambapo yenyewe imekusanya pointi 23 katika mechi 10, Yanga ikiwa kinara ikivuna pointi 27 katika michezo 11 na Azam imekusanya pointi 26 katika mechi 11.
Wakati Simba ikiwa tishio nyumbani, Dodoma Jiji FC imekuwa dhaifu ugenini kwani katika mechi 10 imevuna pointi tano tu.