Simba Queens haishikiki sasa

Dar es Salaam. Simba Queens imeendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika ligi kuu ya wanawake baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 11-0 dhidi ya Mlandizi Queens katika Uwanja wa KMC Complex,Mwenge, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, mabao yalifungwa na Aisha Mnunka aliyeweka kambani mawili, Asha Djafar (hat-trick), Jentrix Shikangwa manne na Precious Christopher.

Huu ni mchezo wa pili timu hizo zimekutana baada ya ule wa mzungukio wa kwanza ambao Simba iliondoka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni.

Hata hivyo, kivutio kikubwa kwenye mchezo huo kilikuwa mshambuliaji wa Simba, Mnunka ambaye alionyesha kiwango bora kwenye mchezo wake wa kwanza tangu arejee katika timu hiyo ambayo aliikacha bila ya kuaga.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita aliibuka kinara wa ufungaji alipotupia mabao 21, alikuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitano, alipoondoka klabuni kiutata huku ripoti zikidai kuna klabu ilimtorosha kwa nia ya kumsajili, licha ya kwamba alikuwa bado ana mkataba na Simba.

Matokeo hayo yanaifanya Simba iendelee kusalia kileleni na pointi 28 huku JKT Queens ikiwa nafasi ya pili na pointi 23 na Mashujaa ikisalia nafasi ya tatu na pointi 18.

Ukiachana na matokeo hayo kuna vita ya wafungaji kwa Shikangwa ambaye ana mabao 14 kwenye mechi 10 nyuma ya Stumai Abdallah wa JKT mwenye nayo 10 na wote wakifunga hat-trick kwenye mchezo wa duru la pili.