Simba, Pamba zatinga 16 bora kibabe Kombe la CRDB

Simba imetinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya leo, Jumanne Machi 11, 2025 kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TMA kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mabao yaliyoipeleka Simba kwenye hatua inayofuata ya mashindano hayo yalifungwa na Valentine Nouma, Lionel Ateba na lingine moja lilikuwa la kujifunga la Sixtus Sabilo.

Kama ambavyo ilitegemewa na wengi, Simba ilitawala mchezo wa jana kwa muda mrefu licha ya kuanza na kikosi ambacho kilikuwa wachezaji sita ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kuanza mara kwa mara kikosini kwa siku za hivi karibuni.

Mohamed Hussein, Fabrice Ngoma, Elie Mpanzu, Kibu Denis, Charles Ahoua na Yusuph Kagoma hawakuanza kikosini na nafasi zao walianzishwa Debora Mavambo, Valentine Nouma, Awesu Awesu, Augustine Okejepha, Ladack Chasambi na Joshua Mutale.

Baada ya kosakosa kadhaa langoni mwa TMA ambayo muda mrefu ilijaza idadi kubwa ya wachezaji katika eneo lake la ulinzi, Simba ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 17 kupitia kwa Valentine Nouma ambaye alikwamisha mpira wavuni kwa shuti la moja kwa moja la faulo lililomshinda kipa Ismail Salehe wa TMA, faulo ambayo ilipatikana baada ya Awesu Awesu kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari la timu hiyo ya Arusha.

Dakika mbili baadaye, Simba ilipata bao la pili ambalo lilikuwa la kujifunga la Sixtus Sabilo aliyekuwa katika harakati za kuokoa mpira wa krosi wa Ladack Chasambi.

Bao hilo lilidumu hadi refa Tatu Malogo alipopuliza filimbi ya mapumziko.

Kipindi cha pili, TMA waliongeza zaidi nidhamu ya kujilinda huku wakishambulia katika nyakati chache wakati huo Simba wakiendelea kushambulia huku wakipoteza nafasi kadhaa walizotengeneza.

Hata hivyo dakika ya 75, Lionel Ateba aliipatia Simba bao la tatu na la mwisho akimalizia krosi ya Kelvin Kijili.

Katika mchezo mwingine, Pamba Jiji imeinyuka Kiluvya United kwa mabao 3-0, mechi ambayo imechezwa katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Mabao ya Pamba Jiji leo yamepachikwa na Mathew Tegis, Ałły Ramadhan na Yonta Camara.

Mchezo wa mwisho leo utakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Kagera ambao utawakutanisha wenyeji Kagera Sugar na Namungo FC na umeanza saa 12:00 jioni.

Hadi sasa timu 14 zimefuzu hatua ya 16 bora ambazo ni Simba, Pamba Jiji, KMC, Bigman, Singida Black Stars, Mbeya City, Mashujaa, Mtibwa Sugar, Stand United, Mbeya Kwanza, Girrafe Academy, JKT Tanzania, Tabora United na Songea United.