Simba na miaka 17 ya milima na mabonde Kombe la Shirikisho Afrika

Dar es Salaam. Baada ya kuiondosha Al Ahli Tripoli ya Libya, Simba imetinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili tangu ilipofanya hivyo msimu wa 2021-2022 ilipoitoa Red Arrows ya Zambia.

Kwenye mchezo dhidi ya Al Ahli Tripoli kutoka Libya, Jumapili, Septemba 22, 2024 Simba ilitoka nyuma kwa bao moja na kupata ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na hivyo kusonga mbele kwenye hatua ya makundi.

Safari ilipoanzia

Imepita miaka 17 tangu  Simba ilipoanza kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2007.

Ni miaka 14 ilisubiliwa kuiona Simba ikitinga hatua ya makundi kwenye kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Red Arrows ya Zambia msimu wa 2021-2022.

Simba ilicheza hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galax ya Botswana.

Kwenye hatua ya makundi Simba ilipangwa na RS Berkane (Morocco), ASEC Mimosas (Ivory Coast) na US Gendermarie ya Niger ambapo Simba ilifanikiwa kwenda hatua ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi ikivuna pointi 10 sawa na RS Berkane iliyokuwa nafasi ya kwanza kwa kwa kanuni ya kupata matokeo bora kwenye mechi mbili dhidi ya Simba.

Kwenye robo fainali, Simba ilikutana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambapo mechi mbili baina yao zilimalizika kwa sare ya bao 1-1 kufuatia Simba kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na  Orlando Pirates kushinda bao 1-0 huko Johannesburg, Afrika Kusini lakini Simba ilitolewa kwenye mikwaju ya penati 4-3.

Simba imecheza michezo 30 ya kombe la Shirikisho Afrika tangu 2007 ikishinda mechi 15, ikitoa sare mechi sita, na kupoteza  mechi tisa.

Edwin Balua akishangilia baada ya kufunga bao la tatu Simba ikishinda 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli

Mabao yaliyofungwa na Kibu Denisi, Leonel Ateba na Edwin Balua yanaifanya Simba kufikisha mabao 45 kwenye Kombe la Shirikisho huku bao pekee la Al Ahli Tripoli lililofungwa na  Agostinho Cristóvão Paciência ‘Mabululu’ linakuwa bao la 35 kutikisa nyavu za Simba.

Agostinho Cristóvão Paciência ‘Mabululu’ akishangilia baada ya kuifungia Al Ahli Tripoli bao la kwanza

Mara ya mwisho Simba kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ilikuwa ni msimu wa mwaka 2021-2022 ilipokuwa chini ya kocha Pablo Franco Martin ambaye kwa sasa anainoa Amazuru inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.

Ushindi dhidi ya Al Ahli Tripoli unaifanya Simba kuingia hatua ya makundi kwa mara ya pili kwenye kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kufanya hivyo mara nne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Safari bado inaendelea

Klabu ya Simba bado inaendelea na safari katika mashindano ya Shirikisho ambapo viongozi na benchi la ufundi wana matumaini ya kuifikisha mbali timu yao wakiwa na malengo ya kufika fainali katika mashindano haya kama walivyo fanya watani wao wa jadi Yanga msimu wa 2022-2023.