LICHA ya kubakiwa na mechi saba kwa upande wa Yanga ukiondoa mchezo wa Jumamosi huku Simba wakibakiwa na mechi nane, mchezo wao wa dabi ndio unaoaminika kama ndio wenye kuamua nani bingwa kati ya watani hao wa jadi, japo hilo sio lazima litokee.
Vinara Yanga baada ya kumenyana na Simba Jumamosi watakuwa wamebakiza mechi saba dhidi ya Tabora United (ugenini), v Coastal Union (nyumbani), v Azam FC (ugenini), v Fountain Gate (ugenini), v Namungo (nyumbani), v Tanzania Prisons (ugenini) na watamaliza dhidi ya Dodoma Jiji (nyumbani)
Simba ina kiporo dhidi ya Dodoma Jiji ambacho bado hakijapangiwa tarehe lakini pia itakuwa na mechi dhidi ya Mashujaa (nyumbani), JKT Tanzania (ugenini), Pamba (nyumbani), KMC (ugenini), Singida Black Stars (nyumbani), KenGold (ugenini) na Kagera Sugar (nyumbani).
Hivyo endapo mmoja kati yao atapata matokeo Jumamosi atabaki na kibarua cha kuchanga karata zake vizuri kwenye mechi zilizobaki ili kujihakikishia kutwaa taji la ligi huku Yanga akitaka kuwajibu watani wao Simba waliotwaa mataji manne mfululizo katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, rekodi ya muda wote inaonyesha Yanga na Simba kila moja imewahi kulitwaa taji la Ligi Kuu Mara tano mfululizo, Yanga ikitangulia kufanya hivyo kuanzia mwaka 1968 hadi 1972, kabla ya Simba kujibu kuanzia 1976 hadi 1980.
Yanga inaongoza msimamo ikiwa imekusanya pointi 58 kwenye mechi 22 ilizocheza wakati Simba ina pointi 54 kwenye michezo 21 waliyocheza kabla ya mchezo wao wa Jumamosi hivyo wameachwa nyuma mchezo mmoja.

Mwanaspoti linakuletea mambo matano ambayo yatakuwa ya tofauti kwenye mchezo wa Jumamosi kutokana na mechi tano zilizopita.
MECHI YA KUAMUA
Yanga itakayokuwa timu mwenyeji katika mchezo wa Jumamosi itaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya kushinda dabi mbili mfululizo dhidi ya wekundu hao wakiwa chini ya kocha aliyepo Fadlu Davids na itashuka dimbani ikiwa inaongoza ligi kwa pointi nne mbele.
Watetezi hao wamecheza mechi moja zaidi ya Simba ambayo ina kiporo dhidi ya Dodoma Jiji, hivyo mchezo wa Jumamosi hautokuwa mwepesi, wanakutana wakiwa hawajaachana sana pointi na kila timu inautazama mchezo huo kama ndio wa kutoa mwelekeo wa mbio za ubingwa.
Katika misimu mitatu iliyopita ambayo Yanga imetwaa ubingwa mfululizo, imekutana na Simba katika mechi ya raundi ya 23 mara mbili na ya kesho itakuwa ni ya tatu kucheza tena mechi ya raundi ya 23 (japo Simba ina kiporo).
Achana na msimu wa 2021/22 ambao ulikuwa wa kwanza kwa Yanga kutwaa ubingwa katika misimu hii mitatu mfululizo iliyopita. Msimu huo, walikutana katika raundi ya 20 huku katika mechi zao 19 za kwanza Simba tayari ilishaachwa kwa pointi nyingi, Yanga ikiwa na 51 na Simba ikiwa na 41.
Msimu uliofuata 2022/23 walikutana katika raundi ya 23, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 2-0. Kabla ya mchezo huo, Yanga ilikuwa na pointi 59 huku Simba ikiwa na 53. Wanajangwani walitwaa taji.
Halafu tena msimu wa 2023/24 pia walikutana raundi ya 23 Yanga ilishinda 2-1. Raundi 22 Yanga ilikuwa imekusanya pointi 56, Simba 52. Mwisho Yanga ikatwaa kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo. Sasa msimu huu Simba anazidiwa pointi 4 ina mchezo mmoja mkononi. Mchezo wa Jumamosi utakuwa ni wa raundi ya 23 Yanga inaongoza ikiwa na pointi 58 dhidi ya 54 za Simba yenye kiporo.
SAFU KIWEMBE
Mzunguko huu watani hao wanakutana wakiwa na safu imara kila upande lakini mabingwa watetezi Yanga wanaonekana kuwa tishio zaidi kutokana na washambuliaji wake kuwa bora kwenye upachikaji wa mabao wakifunga mabao 24 huku Simba wao wakifunga mabao 18.

Yanga wana Prince Dube ambaye amefunga mabao 10 sawa na Clement Mzize huku Keneddy Musonda akitupia kambani mabao matatu na Jean Baleke ambaye ametemwa kikosini na si sehemu ya mchezo amefunga bao moja.
Safu ya ushambuliaji ya Simba inaongozwa na Lionel Ateba akifunga mabao manane sawa na Steven Mukwala wamefunga mabao 16 huku Valentino Mashaka akipachika mabao mawili pekee na kufanya safu yao ifunge mabao 18 kati ya 46 yaliyofungwa na timu hiyo.
Hivyo kwa pande zote mbili timu ambayo itatumia vizuri nafasi watakazotengeneza ndio itakayoibuka na ushindi kwenye mchezo huo, huku safu zote za ulinzi zitakuwa na kazi kubwa ya kufanya kuepusha dhahama kwa makipa wao ambao wote wameruhusu nyavu zao kutikiswa.
AHOUA vs AZIZ KI
Eneo hili kazi yake mama ni kutengeneza nafasi kwa kuhakikisha wanawalisha washambuliaji wao lakini pia wanapopata nafasi ya kufunga wanafanya hivyo. Timu zote zipo vizuri eneo hili, lakini Yanga wachezaji wake wanabebwa na namba.

Eneo hilo ukiachana na Yanga kuwa na namba kubwa kutokana na kuwa na wachezaji wengi ambao hadi sasa wameonyesha uwezo mkubwa, kuna nyota hawa kila upande ambao wamekuwa wakitumika kwenye mambo mengi kama kupiga mikwaju ya penalti na mipira ya kutengwa — Charles Ahoua wa Simba na Stephane Aziz Ki wa Yanga.
Vita yao inakutanisha wachezaji bora watatu wa Ligi Kuu ya Ivory Coast katika misimu iliyopita ambapo Ahoua alikuwa MVP wa 2023/24, Pacome Zouzoua (2022/23) na Aziz (2021/22). Wakati Yanga nyota wao wawili tayari wana uzoefu wa Bongo, Ahoua licha ya kuwa ni msimu wake wa kwanza, amewafunika wawili hao wa Yanga kitakwimu.
Katika vita hiyo, mwamba wao ni Ahoua ambaye amehusika katika mabao 16 akifunga 10 na kutoa asisti sita kwenye dakika 1360 katika mechi 19 alizocheza, wakati Pacome amehusika kwenye mabao 13 akifunga saba na asisti sita akitumika kwenye mechi 20 (dakika 1117), huku Aziz Ki akihusika kwenye mabao 12 akifunga mabao saba na kutoa asisti tano akitumika kwa dakika 1481 kwenye mechi 22.
FADLU vs HAMDI
Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na faida ya kuwa na benchi la ufundi ambalo licha ya kupoteza mechi mbili mfululizo za dabi hii, tayari lina uzoefu na mchezo huo ambao utachora ramani ya ubingwa kwa timu zote mbili.
Fadlu Davids alipokewa na vipigo akianza na Ngao ya Jamii wakati Wekundu walipolala 1-0 na kudondosha taji la kwanza msimu huu, huku bao la ushindi kwa upande wa Yanga likifungwa na Maxi Nzengeli, kabla kipigo kingine cha ligi cha 1-0, bao lililofungwa na beki wake Kelvin Kijiri wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Maxi.

Wakati Fadlu akiingia kwenye mchezo wa Jumamosi kwa kujiuliza nini anapaswa kukifanya kupata matokeo dhidi ya Yanga, kwa upande wa kocha Miloud Hamdi yeye atakuwa na kibarua kuiongoza timu hiyo yenye rekodi nzuri kuendeleza ubabe.
Hamdi tangu amekabidhiwa mikoba ya Sead Ramovic aliyetimkia CR Belouizdad ameiongoza timu hiyo kwenye mechi sita hajapoteza mchezo wowote zaidi ya sare moja dhidi ya JKT Tanzania ugenini.
Hivyo ataingia kwenye mchezo huo akiwa na kibarua cha kulinda rekodi zilizoachwa na makocha waliomtangulia kwenye ushindi wa dabi za hivi karibuni lakini pia akiendelea kusaka rekodi ya kushinda michezo yote iliyosalia baada ya kuanza kwa kishindo.
TOFAUTI YA VIKOSI
Kuna mabadiliko makubwa kwenye vikosi vyote viwili tofauti na misimu ambayo Yanga iliibuka na ushindi.
Katika mechi mbili za Dabi ya Kariakoo ambazo Fadlu amepoteza aliweka wazi kuwa anajenga kikosi. Sasa timu imejipata na ipo katika ushindani wa kuwania taji ikiachwa kwa pointi nne na kiporo kimoja mkononi.
Simba inaonekana kuimarika licha ya upungufu mdogo mdogo ilionao, lakini imekuwa timu ambayo inaonyesha ushindani mkubwa kuanzia ndani hadi katika michuano ya kimataifa.
Kwa upande wa Yanga ambayo msimu huu licha ya kushinda mechi mbili dhidi ya Simba, ilianza msimu kwa kusuasua tofauti na misimu miwili nyuma imetimua makocha wawili ndani ya msimu mmoja na kufanya ifundishwe na makocha watatu.
Ilianza na Miguel Gamondi baada ya kushindwa kuendana na kasi hasa kimataifa ambapo wameondolewa hatua ya makundi tofauti na msimu uliopita nyuma, wakamchukua Ramovic ambaye pia alidumu siku chache na sasa timu ipo chini ya Hamdi.