
KIKOSI cha Simba kinashuka katika Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam kusaka tiketi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Mbeya City inayoshiriki Ligi ya Championship mechi inayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali baada ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiitoa Al Masry ya Misri kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2.
Mchezo wa Simba dhidi ya Mbeya City utazikumbushia timu hizo zilipokutana mara ya mwisho Januari 18, 2023 kwenye Ligi Kuu Bara. Katika mchezo huo wa msimu wa 2022-2023 uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilishinda mabao 3-2 yaliyofungwa na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyefunga mawili na Pape Sakho. Kwa sasa nyota hao hawapo Simba.
Kwa upande wa mabao ya Mbeya City msimu huo ambao ndio ulikuwa wa mwisho kucheza Ligi Kuu yalifungwa na Richardson Ng’ondya na Juma Shemvuni. Simba inayonolewa na Fadlu Davids, safari yao katika Kombe la FA ilianzia hatua ya 64 kwa kuifunga Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro mabao 6-0, hatua ya 32 bora ikaichapa TMA ya Arusha mabao 3-0. Hatua ya 16 bora, Simba ikakutana na Bigman ikaichapa mabao 2-1.
Mbeya City ilianza kwa kuitoa Mapinduzi ya Mwanza kwa mabao 2-1. Baada ya hapo ikakutana na Azam ikaitupa nje kwa penalti 4-2 baada ya kufungana bao 1-1, kisha ikaiondosha Mtibwa Sugar kwa mabao 2-1.
Katika mchezo huu, nyota wa kuchungwa kwa Mbeya City ni William Thobias aliyefunga mabao tisa msimu huu ya Championship, huku akichukua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Machi. Mwingine ni Eliud Ambokile aliyetupia kambani mabao manane.
Faraji Kilaza Mazoea mwenye mabao sita ni nyota mwingine wa kuchungwa kutokana na uwezo wa kufumania nyavu aliokuwa nao, huku kwa upande wa Simba ikiendelea kuwategemea washambuliaji Leonel Ateba na Steven Mukwala.
Mukwala mwenye mabao tisa kwenye ligi, huku Ateba akiwa nayo manane ni miongoni mwa washambuliaji wa kutegemewa katika kikosi hicho kinachosaka taji hilo baada ya kulichukua mara ya mwisho 2020-2021.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha wa Mbeya City, Malale Hamsini alisema anaiheshimu Simba kutokana na ubora wa wachezaji iliokuwa nao, huku akiweka wazi kitendo cha kuiondosha Azam FC kimewapa hali nzuri ya kujiamini wachezaji.
“Tunaenda kukutana na mchezo mwingine mgumu lakini tumejiandaa kukabiliana na changamoto iliyokuwa mbele yetu, wachezaji wote wako katika afya nzuri ya kimchezo na tunashukuru tumepata nafasi ya kufika mapema kuzoea hali ya hewa,” alisema.
Mshindi wa mchezo huo, nusu fainali atakutana na Singida Black Stars au Kagera Sugar zitakazokutana Jumatatu hii.