Simba Mafinga wakataa uteja wa Dabi, wawataja Mpanzu na Ateba

UONGOZI mpya wa Simba, tawi la Mafinga mkoani Iringa umesema kazi ya kwanza katika majukumu yao ni kuondoa uteja pale watakapokutana na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Jumamosi, wiki hii.

Simba inatarajia kukutana na Yanga katika mchezo unaopigwa Machi 8 katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, huku rekodi zikiwabeba watani wao wa Jangwani ambao wamefululiza ushindi katika mechi nne.

Hadi sasa Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu kwa pointi 58 wakiwa mbele kwa mchezo mmoja dhidi ya Simba walio nafasi ya pili kwa alama 54 baada ya mechi 21.

Timu hizo zinakutana ikiwa Yanga kashinda mara nne mfululizo ikiwamo kipigo kizito cha 5-1 walipokutana Novemba 5, 2023 na Jumamosi hii miamba hiyo itamenyana huku Yanga ikitaka kuendeleza rekodi, Simba wakihitaji kufuta uteja.

Akizungumza baada ya uchaguzi wa tawi hilo, Mwenyekiti mpya, Mathew Mkumbo amesema wamechoshwa na vipigo mfululizo dhidi ya watani wao hao, hivyo Machi 8 inyeshe mvua liwake jua lazima Yanga akae zaidi ya mabao mawili.

Amesema ubora wa kikosi chao kwa wachezaji wote, yeyote atakayepangwa kuanza katika mechi hiyo anaweza kuamua dakika 90, huku akiwataja Lionel Ateba na Elie Mpanzu kuwasha moto Taifa.

“Hatukubali tena kufungwa na watani, tumejipanga ndani na nje ya uwanja kuhakikisha Yanga anakufa mabao mawili, Mpanzu, Ateba hata Kibu yeyote anaweza kuwazima watani”

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha Mnyama anatakata Taifa, wanatarajia kufurika Dar es Salaam ambapo zaidi ya mashabiki 3000 kutoka Mafinga watashuhudia mbungi hiyo.

“Tayari mabasi yameandaliwa na muitikio wa mashabiki ni mkubwa, kumbuka tawi letu ni la pili kwa ukubwa nchini likianza Misenyi (Kagera), tutafurika pale Taifa kwa lengo moja tu, kumuua mtani” ametamba kiongozi huyo.

Kwa upande wake mwanzilishi wa tawi hiyo, Dickson Mwaipopo amewaomba mashabiki wa Wekundu kujitokeza zaidi katika mchezo huo ili kuipa nguvu Simba kuweza kushinda mechi hiyo.

“Yanga lazima wafungwe, tunaye Mpanzu anawasha sana moto, niwaombe wanachama na mashabiki kujitokeza kwa wingi katika dabi hiyo tuweze kupata ushindi” amesema Mwaipopo.

Katika uchaguzi huo, Mkumbo alichaguliwa nafasi ya Mwenyekiti, Peter Raurtus (Makamu Mwenyekiti), Henry Nyilenda (Katibu) na Mhasibu Mary Momo.

Kwa upande wa wajumbe waliochaguliwa ni Emanuel Ng’umbi, Sebastian Sanga, Onely Mlandali na Meriana Mtisi ambao wataongoza wenzao kwa miaka minne.