Simba kwenye mtihani mgumu Kwa Mkapa leo

Simba inatupa karata muhimu leo nyumbani dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili iweze kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika mchezo wa kwanza uliofanyika Libya, Jumapili iliyopita.

Mechi hiyo itachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00.

Kinyume na matokeo ya ushindi, Simba inaweza kujikuta inaaga mashindano hayo ikiwa mechi hiyo ya leo itamalizika kwa matokeo ya sare ya mabao na kama itaisha kwa sare tasa, kwa mujibu wa kanuni, mshindi itapatikana kwa mikwaju ya penalti.

Simba inasaka tiketi ya kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano ya klabu Afrika kwa mara ya tano mfululizo baada ya kufanya hivyo katika misimu ya 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Simba ilitinga hatua ya makundi mara moja ambapo ni msimu wa 2021/2022 iliposhia hatua ya robo fainali ambayo ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi baina yao.

Ili mpango huo wa kuitupa nje Al Ahli Tripoli ukamilike leo, Simba inapaswa kuhakikisha safu yake ya kiungo inatengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao na ile ya ushambuliaji kuzitumia vyema ili ipate ushindi ambao utaivusha kwenda hatua inayofuata.

Katika mchezo wa kwanza Simba ilitengeneza nafasi chache za mabao huku ikishindwa kuzitumia hadi kupelekea imalize mechi hiyo ikiwa haijapiga shuti hata moja lililolenga lango.

Mawinga wa Simba leo wanapaswa kuwa katika kiwango bora ili kwanza kuifanya timu yao kutengeneza idadi kubwa ya mashambulizi kutokea pembeni jambo ambalo halikuonekana katika mchezo wa kwanza lakini pia ili kuwapunguza kasi walinzi wa pembeni wa Al Ahli Tripoli ambao wamekuwa silaha ya timu hiyo ya Libya katika kutengeneza mashambulizi.

Katika mchezo wa kwanza, mawinga wa Simba, Joshua Mutale na Edwin Balua walionekana kupoteza mipira mara kwa mara lakini pia kuna nyakati walikuwa wanachelewa kurudi nyuma kusaidia ulinzi pindi Simba ilipokuwa inashambuliwa jambo ambalo liliipa kazi ngumu safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Silaha kubwa ambayo Simba inaitegemea katika mechi ya leo ni safu yake ya ulinzi ambayo msimu huu imeonekana kutoruhusu kirahisi wapinzani kufumania nyavu zao.

Katika mechi tano za mashindano ambazo Simba imecheza msimu huu, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu huku mara nne ikimaliza bila kufungwa bao.

Al Ahli Tripoli yenyewe katika mechi tano zilizopita, imeruhusu bao katika mechi tatu ambapo imefungwa idadi ya mabao matatu.

Mchezo huo utachezeshwa na refa Abdoulaye Manet kutoka Guinea mwenye umri wa miaka 34.

Manet atasaidiwa na Waguinea wenzake ambao ni Sidiki Sidibe, Yamoussa Sylla na Bangaly Konate.

Huo ni mchezo wa kwanza wa mashindano ya klabu Afrika kwa Manet kuchezesha ambapo kabla ya hapo kitu pekee cha kujivunia kwa refa huyo kilikuwa ni kuwa refa wa akiba.

Ikiwa Simba itaingia hatua ya makundi leo itajihakikishia kitita cha Dola 100,000 (272 milioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Al Ahli Tripoli sio timu ya kinyonge ugenini na hivyo Simba inapaswa kuwa na tahadhari kubwa katika mchezo wa leo ili kutowapa wapinzani wao fursa ya kuwaadhibu.

Katika mechi 10 za kimataifa zilizopita ambazo Al Ahli Tripoli imecheza ugenini, timu hiyo imeibuka na ushindi mara nne, kutoka sare mbili na kupoteza michezo minne.

Ardhi ya Tanzania imekuwa ni mahali pagumu kwa timu pinzani pindi zikabilianapo na Simba kwenye mashindano ya kimataifa ambapo mara nyingi zimekuwa zikipokea vichapo.

Hilo linaweza kudhihirishwa na michezo 10 iliyopita ya mashindano ya kimataifa ambayo Simba imecheza ikiwa nyumbani ambapo imeibuka na ushindi mara sita, kutoka sare mbili na kupoteza mechi mbili.