Simba kuivaa TMA hatua ya 32 bora FA

Baada ya kushindwa kuchezwa kwa mechi ya Dabi ya Kariakoo wikiendi iliyopita dhidi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara, leo jioni Simba inatarajiwa kushuka uwanjani kuvaana na TMA Stars ya Arusha ukiwa ni mchezo wa hatua ya 32 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA).

Hii ni kati ya mechi tatu za michuano hiyo zinazopigwa leo, ukiwamo ule wa Kiluvya United dhidi ya Pamba Jiji na Kagera Sugar itakayokuwa wenyeji wa Namungo, huku Simba ikiwa wenyeji dhidi ya maafande wa TMA iliyopo Ligi ya Championship kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Mechi zote zimepangwa kupigwa jioni na washindi watasonga mbele kuingia barua ya 16 bora itakayoanza Alhamisi kwa mchezo kati ya Mbeya City iliyoitoa Azam dhidi ya Mtibwa Sugar.

TMA Stars inayofundishwa na kocha Mohamed Ismail ‘Laizer, ipo nafasi ya tano katika Ligi ya Championship itashuka uwanjani kukabiliana na Simba iliyopo nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara na ikiwa na kikosi chenye wachezaji wenye uchu wa kufumania nyavu, Leonel Ateba, Jean Ahoua na Steven Mukwala.

Huu ni mchezo unaoweza kuwa wa upande mmoja kufuatia ubora wa Simba na namna ambavyo Kocha Laizer amekizungumzia kikosi chake kinachopambana Championship kuhakikisha kinafanya vizuri, lakini lolote linaweza kutokea.

Kocha Laizer amefichua mwenendo wa kikosi chake sio mbaya ingawa changamoto ya kuruhusu mabao ndiyo kazi kubwa anayopambana nayo.

Kutokana na hilo, mabeki wa TMA wana kazi kubwa ya kuwazuia Simba ambao mchezo uliopita wa 64 Bora iliichapa Kilimanjaro Wonders mabao 6-1.

Ubora wa safu ya ushambuliaji ya Simba ndio unaiweka katika mtihani mgumu TMA iliyoruhusu mabao 20 katika Championship msimu huu kupitia mechi 22, ilihali Simba katika Ligi Kuu imefunga mabao 46 na kufungwa manane tu, ikidhihirisha ipo imara katika kulinda na kushambulia.

Hata hivyo, TMA Stars katika michuano hii hatua ya 64 nayo haipo kinyonge kwani ilitoa onyo kwa kuichapa Leopards mabao 5-1, hivyo tunaweza kuweza kushuhudia maajabu.

Hesabu za Simba ni kuona inafanya vizuri hatua hii na kufuzu 16 bora ili kuuendea ubingwa wa michuano hiyo unaoshikiliwa na Yanga ambao mara ya mwisho wa kuutwaa ilikuwa msimu wa 2020/21.

TMA Stars haijawahi kubeba ubingwa wa michuano hiyo, nayo inataka kuweka rekodi mpya huku ikifahamika kwamba mshindi baina yao anakwenda kucheza hatua ya 16 Bora dhidi ya BigMan iliyoichapa TZ Prisons kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 katika dakika 90 za mchezo huo.

Baadhi ya nyota wa TMA Stars wanaobeba matumaini ya kikosi hicho ni Bastian Joseph, Abdul Aziz Shahame na Sixtus Sabilo aliyewahi kucheza JKT Tanzania, Namungo na Mbeya City.

Kocha Laizer ameliambia Mwanaspoti, anachoshuruku ni kwamba wachezaji 28 aliosafiri nao kutoka Arusha hadi Dar kuifuata Simba wapo katika hali nzuri, wanachosubiri ni muda wa mechi ufike waingie uwanjani kupambana kikubwa.

“Tumesafiri kutoka Arusha kuja Dar, tupo vizuri, tunasubiri muda wa mechi ufike tukacheze. Ukiangalia hali ya wachezaji wangu wote 28 tuliosafiri nao wapo katika hali nzuri.

“Nafahamu tunakutana na Simba ambayo ni timu kubwa, hivyo na sisi tumejiandaa kucheza kikubwa,” alisema Laizer.

KILUVYA UTD v PAMBA

Kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro saa 10:00 jioni, wenyeji Kiluvya United watawakaribisha Pamba Jiji katika mchezo mwingine wa hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo.

Pamba Jiji ambayo hatua ya 64 Bora ilifunga Moro Kids bao 1-0, katika safari yake kwenda kucheza dhidi ya Kiluvya United, msafara wake ulipata ajali lakini hakukuwa na madhara makubwa waliyopata wachezaji wala viongozi wao ndiyo maana mechi inapigwa leo.

Moto waliouwasha Kiluvya United katika hatua ya 64 Bora kwa kuichapa African Lyon mabao 4-0, unaweza kuwa tishio kwa Pamba Jiji, hivyo ni mechi ya kuitazama kwa umakini mkubwa.

Pamba Jiji haipo vizuri kwenye Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya 13 na pointi zake 22 baada ya mechi 23, imetoka kuchapwa na Kagera Sugar ugenini, hivyo mchezo huu unaweza kutumika kuwafuta machozi mashabiki wao na kufufua matumaini ya kufikia malengo yao ya kutoshuka daraja lakini kufanya vizuri michuano hii kwani bingwa wake ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kiluvya United nayo si kwamba ipo vizuri sana Ligi ya Championship, bali inajitafuta ikishika nafasi ya 12 na pointi zake 19 katika michezo 22.

KAGERA v NAMUNGO

Mchezo wa mwisho leo utachezwa saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera ambapo wenyeji Kagera Sugar wanaikaribisha Namungo.

Hizi ni timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na msimu huu tayari zimekutana katika duru la kwanza uwanjani hapo Kaitaba matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.

Msimu uliopita, Aprili 2, 2024 timu hizo zilikutana katika michuano hii hatua ya 16 Bora, mechi ikichezwa Uwanja wa Majaliwa ambapo ni nyumbani kwa Namungo na wenyeji kushinda kwa penalei 5-3 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.

Safari hii wanapokwenda kukutana, Kagera wana nafasi ya kulipa kisasi nyumbani kwao.

Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana jumla mara 12 katika michuano yote, Kagera ikishinda mechi mbili, wakati Namungo imeshinda sita, sare nne.

Katika hatua iliyopita, Namungo iliifunga Tanesco 2-1, wakati Kagera ikiichapa Rhino Rangers 1-0.

Kwa mujibu wa kanuni za mechi za raundi hizo za awali, timu zikitoka sare ndani ya dakika 90 mshindi atapatikana kupitia mikwaju ya penalti.

Ukichana na mechi moja ya jana kati ya Fountain Gate dhidi ya Stand United, hadi sasa timu zilizofuzu hatua ya 16 bora ni Singida Black Stars, KMC, Mbeya City, Mtibwa Sugar, JKT Tanzania, Mbeya Kwanza, Tabora United, Mashujaa, Giraffe Academy, Songea FC na Big Man.

Michuano hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja wa 32 Bora kati ya watetezi Yanga dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *