
Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally amesema tayari timu hiyo imejiandaa na safari ya kwenda Misri kwaajili ya mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry unaotarajiwa kuchezwa Aprili 02, 2025.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Ahmed amesema;
“Kikosi kitaondoka nchini alfajiri ya tarehe 28 kuelekea Misri. Wachezaji wetu waliokuwa Taifa Stars wataungana na timu nchini Misri. Camara na Mukwala tayari wamewasili nchini kujiunga na wachezaji wenzao kwa ajili ya maandalizi ya safari.”
“Kila Mwanasimba atambue kwamba pamoja na mipango tuliyonayo lakini lazima tujipange, lazima tujiandae na hasa kama timu yenyewe inatokea Misri. Ukiangalia michuano ya Afrika ilivyo utaona kwamba Misri ndio nchi iliyoingiza timu nne kwenye robo fainali.”
“Tunakwenda kucheza na Al Masry tukijua tunakwenda kucheza mechi ngumu kwelikweli lakini dhamira tuliyojiwekea ni kufuzu nusu fainali.”
“Niwatoe hofu kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa umeshafanyiwa ukaguzi. Bado majibu hayajatoka lakini katika mazungumzo wanasema kuna maboresho makubwa kwenye uwanja ukilinganisha na mara ya mwisho walipofanya ukaguzi hivyo kuna nafasi kubwa ya kucheza kwenye uwanja huo. Na wote mnakumbuka kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali alivyosema kwamba uwanja upo tayari. Hatuna muda wa kusubiri tunafanya maandalizi.
Ameongeza kuwa kwa mchezo utakaochezwa Kwa Mkapa ambao utakuwa ni Aprili 9, utakuwa na viingilio hivi:
-Mzunguko – 5,000,
-Orange – 10,000,
-VIP C – 15,000,
-VIP B – 30,000,
-VIP A – 40,000,
-Platinum – 150,000 na
– Tanzanite – 250,000.
Ambapo tiketi zimekwisha anza kuuzwa.
“Mechi hii tunataka kuingiza mashabiki kati ya 50,000 hadi 60,000 hivyo tutafanya hamasa kubwa, mtaa kwa mtaa ili kuwahamasisha Wanasimba kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo muhimu. Safari hii tutatembelea matawi mengi sababu tunataka watu wengi waje uwanjani.”