
Simba Queens iko kwenye mpango wa kuachana na Kocha Mkuu, Yussif Basigi mwishoni mwa msimu huu kutokana na kile alichokionyesha Ligi Kuu kutowaridhisha mabosi wa timu hiyo.
Kocha huyo aliyejiunga na Simba akitokea Hasacaas Ladies ya Ghana na ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye ligi, amepoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga Princess na sare mmoja dhidi ya JKT na ameshinda 12.
Basigi alichukua mikoba ya Juma Mgunda aliyebeba ubingwa wa WPL msimu uliopita bila ya kupoteza mchezo wowote akiifunga Yanga na JKT nyumbani na ugenini, kabla ya kutimkia Namungo.
Kwa taarifa ilizozipata Mwanaspoti, Simba inamsubiria amalize mechi nne zilizosalia kisha iachane naye kwani alisaini mkataba wa mwaka mmoja.
Chanzo kililiambia gazeti hili viongozi wamejadiliana na kuona kocha huyo hataweza kufikia malengo waliyojiwekea tangu msimu unaanza ikiwemo kuchukua kombe la Ngao ya Jamii lililoenda kwa wanajeshi wa JKT Queens.
“Ligi bado inaendelea lakini kwa inavyoonekana kuna uwezekano hata ubingwa wa ligi tukaukosa, viongozi tumeshauriana na kuona hakuna haja ya kuendelea naye, tusubiri tu amalize mkataba wake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tuligundua shinda tangu mechi na Ceasiaa tuliyopata bao moja dakika za jioni, tulimwita kocha pale pale uwanjani na kumuuliza kama kuna shida sehemu akajibu hakuna, kwa hiyo maamuzi ni hayo.”