
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imebadili uwanja na muda wa kuanza kwa mchezo namba 167 wa Ligi Kuu ya NBC baina ya Simba na Azam ambao ulipangwa kufanyika kwenye Uwanja wa KMC Complex, Februari 24, 2025 kuanzia saa 10:00 ambapo sasa utafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku hiyohiyo kuanzia saa 1:00 usiku.
Taarifa iliyotolewa na TPLB leo imesema kuwa sababu ya mabadiliko hayo ni kutoa fursa kwa mashabiki wengi kutazama.
“Sababu ya mabadiliko hayo ni kutoa nafasi kwa mashabiki wengi zaidi kuhudhuria mchezo huo ambao ni moja ya michezo mikubwa ya Ligi Kuu ya NBC inayovuta hisia za watu wengi.
“Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 60,000 umekuwa ukitumika kwa michezo mingi mikubwa na inayohusisha mashabiki wengi zaidi.
“Klabu shiriki (Simba na Azam) pamoja na wadau wengine wa mchezo huo wametumiwa taarifa rasmi ya mabadiliko haya na maandalizi yake yanaendelea vizuri yakiwemo mazingatio ya kiusalama. Bodi inawatakia wadau wote maandalizi mema ya mchezo huo maarufu kwa jina la ‘Mzizima Derby’,” imefafanua taarifa ya TPLB.
Kuhamishwa kwa mechi hiyo kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa kunafanya mechi zote mbili baina ya timu hizo kwenye Ligi Kuu msimu huu kutochezwa katika viwanja vyao ambavyo vinatumia kwa mechi za nyumbani.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina yao msimu huu ilichezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar badala ya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 ambao yalifungwa na Leonel Ateba na Fabrice Ngoma.
Ikumbukwe katika mechi tano zilizopita baina ya timu hizo, Simba imepata ushindi mara mbili, Azam imeshinda moja na zimetoka sare mara mbili.