
LIMEBAKIA bao moja ili itimie ndoto ya mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah anayetamani amalize msimu kwa mabao kuanzia 10, anaamini katika mechi mbili zilizosalia dhidi ya Tabora United na Fountain Gate linaweza likatokea hilo.
Sillah ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao manane kwa sasa anamiliki mabao tisa, alisema mechi za mwishoni zimekuwa ngumu, lakini akipata nafasi ya kucheza atapambana kadri awezavyo ili kufikisha idadi hiyo.
“Unaweza ukaona limebakia bao moja ni kitu rahisi, ukweli ni kwamba mechi zilizosalia na timu tunazokutana nazo zinapambania nafasi katika msimamo wa Ligi Kuu, hivyo tunahitaji kuongeza nguvu zaidi ya mapambano,” alisema Sillah na kuongeza;
“Ingawa jambo la msingi ni timu kupata matokeo mazuri kwa maana nikiona mchezaji mwenzangu yupo eneo la kufunga nikiwa na mpira mguuni nitampa pasi yeye na siyo kujiangalia binafsi.”
Kilichomfurahisha zaidi msimu huu ni ushindani wa ligi uliyochangia wachezaji kucheza kwa viwango vya juu, vilivyoleta ugumu wa kutopata matokeo kirahisi kwa mechi za nyumbani na ugenini.
“Ligi ya Tanzania ni bora, kila unapopata nafasi ya kucheza lazima ujitathimini jinsi ya kuboresha kiwango kitakachokusaidia kulinda nafasi anayopata kikosi cha kwanza,” alisema.