Sillah: Hivi ndivyo Ligi inavyotakiwa

ACHANA na mabao mawili aliyofunga dhidi ya KMC na kumfanya afikishe matano katika Ligi Kuu Bara, mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah amesema amefurahishwa na ushindani uliopo tangu kuanza kwa duru la pili, akisema ndivyo ligi inavyotakiwa.

Sillah alifunga kila kipindi wakati Azam ikishinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na kuifanya timu hiyo ifikishe pointi 39 baada ya mechi 17 ikiwa nyuma ya Simba yenye 44 ikiwa ni tofauti na alama tano, huku Yanga ikiwa kileleni na pointi 45.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Sillah ambaye ni raia wa Gambia alisema anafurahi kufunga mabao na kuisaidia timu kwani inamuongezea nguvu zaidi, lakini hali ya ushindani katika Ligi Kuu inamvutia akisema ndivyo inavyotakiwa kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

“Ligi imechangamka kila timu inataka ushindi, hivyo kitendo cha timu zingine kupata sare, kufungwa kushinda kinazidi kufanya msimamo kubadilika kila wakati kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya mwisho,” alisema na Sillah.

“Kuhusiana na mechi tuliyocheza dhidi ya KMC na kushinda mabao 2-0 imetusaidia kuendelea kujiimarisha nafasi ya tatu, huku tukiendelea kupambana kupanda juu zaidi na hilo linawezekana.”

Alisema haukuwa mchezo rahisi kilichowasaidia ni ushirikiano wa timu na pia imemsaidia kuongeza idadi ya mabao kutoka matatu hadi matano. Sillah msimu uliopita alimaliza na mabao manane na malengo yake msimu huu ni kumaliza na mabao si chini ya 10, akisisitiza atapambana kadri awezavyo ili kulitimiza hilo.

“Ni msimu mgumu kiushindani lakini haunizuii kupambania ndoto zangu kwanza timu kufanya vizuri na mimi kuandika rekodi za kufunga mabao mengi ni kitu ninachotamani kukiona kinatokea” alisema Sillah aliyekuwa akihusishwa kutaka kumtika klabuni hapo kwenda AS Vita ya DR Congo.