
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah amesema kwa namna Ligi ya Tanzania ilivyo ngumu na ushindani wa juu inastahili kutajwa kati ya zilizo bora barani Afrika ambapo kwa sasa ipo nafasi ya nne.
Sillah alisema tangu aanze kucheza Ligi Kuu msimu uliopita, huu ndio msimu bora kwake kwa kiwango binafsi na ushindani wa mechi kwa ujumla, unaowasaidia wachezaji kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzisaidia timu zao.
“Ingawa hatujafikia malengo ya kuchukua ubingwa kama ilivyokuwa matarajio yetu wakati tunauanza msimu huu, hilo halitukatishi tamaa kuendelea kupambana na kuzidi kucheza kwa viwango vya ushindani dhidi ya timu pinzani hadi ligi itakapomalizika,” alisema Sillah na kuongeza;
“Katika Afrika ukitaja Ligi Bora na ngumu kuacha kuitaja Tanzania ambayo imekuwa kivutio kwa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja kuicheza kwa mafanikio makubwa na wengine wamefanikiwa kwenda mbali zaidi baada ya kufanya vizuri hapa.”
Msimu wa kwanza 2023/24, Sillah alifunga mabao manane kupitia mechi dhidi ya Yanga (Yanga 3-2, Oktoba 2023 ), (Azam 2-1 Yanga, Machi 13), (Azam 5-0 KMC, Desemba 7, 2023),(KMC 0-4 Azam, Septemba 19) kisha kuzifunga pia Geita Gold, Mashujaa na Mtibwa Sugar.
Sillah tayari kayafikia mabao manane ya msimu uliyopita na sasa katika mechi tatu zilizosalia dhidi ya Dodoma Jiji, Tabora United na Fountain Gate alisema anatamani afikishe angalau mabao 10.