Siku ya Kimataifa ya Watoto imeadhimishwa duniani huku mauaji ya watoto wa Gaza na Lebanon yanayofanywa na utawala wa Kizayuni yakiendelea bila huruma, suala ambalo pia limeibua wasiwasi kwa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF.
James Elder, Msemaji wa UNICEF amewahutubu walimwengu kwa mnasaba huu kwa kuwaambia: “Mauaji ya watoto huko Gaza na Lebanon yamekuwa jambo la kawaida, na hali hii ya kawaida ni hatari kubwa.”
Amesema: Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, zaidi ya watoto 200 wameuawa na wengine 1,100 wamejeruhiwa nchini Lebanon, wakati ni wazi kuwa mauaji ya watoto kuchukuliwa kuwa jambo la kawaida ni hatari kubwa.”
Tangu kuanza vita vya Gaza, zaidi ya watoto 15,000 wa Kipalestina wameuawa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa. Watoto wengi katika maeneo tofauti ya Gaza pia wako katika hatari ya kuuawa kutokana na njaa. Kulingana na takwimu zilizochapishwa karibuni, watoto wapatao 4,000 wa Kipalestina wamekufa kutokana na njaa, na idadi kubwa miongoni mwao wako hatarini kutokana na makali ya njaa, magonjwa, kuhamahama makazi yao na uhaba wa mahitaji ya kimsingi.
Umoja wa Mataifa unasema mashambulizi ya Israel yamegeuza Gaza kuwa “makaburi” ya watoto katika mwaka mmoja wa vita. Hii ni katika hali ambayo vifo vya watoto wa Gaza haviathiri tena pakubwa maoni ya umma, ambapo hata kuchapishwa mara kwa mara picha za watoto wanaouawa kinyama na Wazayuni kwenye vyombo vya habari sasa kunachukuliwa kuwa jambo la kawaida lisiloamsha hisia kali za watu.
Mauaji ya watoto wa Kipalestina yanaedelea huku Mkataba wa Haki za Watoto, ambao Israel pia imeutia saini ukisisitiza rasmi na kwa uwazi haki ya dhati ya watoto kuishi, ambapo moja ya vipengele vyake, kinasisitiza udharura wa kuzuiwa ukatili na kuandaliwa vifaa vya msingi kwa ajili ya maisha ya watoto. Hata hivyo si tu kwamba mkataba huu hauzingatiwi hata kidogo katika vita vya Gaza, bali kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za haki za binadamu kuhusiana na jinai za utawala ghasibu wa Israel kimechochea kuendelea mauaji ya wanawake na watoto wa Kipalestina yanayofanywa bila huruma na utawala wa Kizayuni.

Ismail Baqaei Hamaneh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwa mnasaba wa madhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto kwamba: “Novemba 20, Siku ya Kimataifa ya Watoto, ni ukumbusho wa haki ya watoto wote kuishi kwa amani na usalama. Licha ya sheria zote za kimataifa, lakini watoto wa Gaza na Lebanon sio tu wanauliwa kwa makusudi katika vita, bali hata wale walio hai wanaishi katika hofu ya vita, bila makazi na bila dawa na huduma za afya.”
Kuakisiwa mauaji ya watoto na hali ya kusikitisha ya maisha ya maelfu ya watoto huko Gaza katika vyombo mbalimbali vya habari hakujaweza kuhamasisha serikali nyingi za dunia kuchukua hatua dhidi ya ukatili na ukandamizaji ambao wamekuwa wakifanyiwa watoto hao. Kama tunavyoona, serikali za nchi za Magharibi zinaendelea kuiunga mkono Israel licha ya mauaji hayo ya kusikitisha dhidi ya wanawake na watoto wasio na hatia.
Anas al-Sharif, mwandishi wa habari wa Palestina, amechapisha picha za watoto waliofariki dunia kwa njaa huko al-Tafa, mashariki mwa Gaza. Wakati fulani nyuma, alielezea hali ya kusikitisha ya shule moja iliyolipuliwa na Israel, na kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kama ifuatavyo: Nilipofika eneo la mauaji, uwezo wangu wa kusema ulitoweka na nikashindwa kuzungumza. Nimechoka na kujawa na maumivu kutokana na wingi wa viungo vya mwili na damu nilizoona leo zimetapakaa kila sehemu.”
Gazeti la Kiingereza la Guardian pia limeandika kuhusiana na suala hili kwamba: “Tumepokea ripoti kutoka kwa madaktari wa Gaza ambazo zinaonyesha kuwa, kinyume na madai ya jeshi la Kizayuni, walenga shabaha na ndege zisizo na rubani za utawala huu zinawalenga watoto “moja kwa moja”. Tarehe 20 Novemba Siku ya Kimataifa ya Watoto inaadhimishwa duniani huku watoto wa Gaza sio tu hawana fursa ya kusherehekea, bali hata mateso yao yanaonekana kuwa ya kawaida kwa vyombo vingi vya habari vya Magharibi, jambo ambalo linawatia wasiwasi pia maafisa wa UNICEF.
Ukweli wa mambo ni kwamba mauaji na mateso dhidi ya watoto wasio na hatia wa Kipalestina yamesababisha majeraha makubwa katika dhamiri ya mwanadamu. Umefika wakati wa jamii ya kimataifa kuwakomesha wahusika wa jinai hizi za kutisha dhidi ya watoto wa Kipalestina.