Leo tarehe Novemba 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kupiga Marufuku Ukatili dhidi ya Wanawake. Hii ni katika hali ambayo wanawake katika nchi nyingi za dunia bado wako chini ya ukandamizaji, dhulma na unyanyasaji, hali ambayo ni mbaya zaidi katika maeneo ya vita kama Ukanda wa Gaza.
Mwaka huu, Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake inaadhimishwa katika hali ambayo kauli mbiu kuhusu kuheshimwa haki za wanawake imekuwa ikipigiwa makelele kwa miongo kadhaa, na bado haki zao za msingi zinakanyagwa katika nchi nyingi za dunia na kuhesabiwa kuwa waathirika wakuu wa vita, kama ilivyo hali ya wanawake wa Kipalestina jambo ambalo linaumiza moyo wa kila mtu aliye na dhamiri huru.
Kuhusiana na hilo, Ismail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba: “Katika Siku ya Kimataifa ya Kupiga Marufuku Ukatili dhidi ya Wanawake, tukumbuke ukatili mkubwa uliosababishwa na miongo kadhaa ya ukatili, uvamizi na mauaji ya kimbari ya kikoloni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu.” Baqaei ameelezea kiwango cha ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake na wasichana huko Gaza kuwa ni jambo lisilo na mfano wake na la kushtua na kusema: “Katika mwaka uliopita, makumi ya maelfu ya wanawake na wasichana wa Kipalestina wameuawa au kujeruhiwa, ambapo akina mama, wanawake na wasichana katika eneo hilo wanakabiliwa na hatari ya njaa na kuhamishwa kwa lazima kutoka makazi yao.”
Mwaka mmoja ukiwa umepita tokea kuanza vita vya Gaza, hali ya wanawake na watoto katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni mbaya na ya kusikitisha sana. Reem al-Salem, Ripota wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake amesisitiza katika ripoti yake kuwa: “Idadi kubwa ya wafanyakazi wa nyanjani hawapati maneno sahihi ya kuelezea hali ya kusikitisha ya Wapalestina huko Gaza na machungu, mateso na ugaidi wanaofanyiwa huko Gaza ambapo utawala katili wa Israel inalenga kwa makusudi wanawake na watoto. Zaidi ya asilimia 70 ya Wapalestina waliouawa kidhalimu ni wanawake na watoto. Wanakabiliwa na jinai za kivita kwa sababu tu wao ni wanawaka wa Kipalestina.

Wanawake wa Gaza wanapitia hali ngumu, wengi wao wakiwa wamepoteza waume na watoto wao. Wengi wanakabiliwa na hatari ya njaa na wala misaada ya kibinadamu hairuhusiwi kuingia katika ukanda huo. Wanawake wajawazito wanalazimika kujifungua katika mazingira ya mashambulizi ya mabomu na ukosefu wa huduma za kimsingi kabisa za matibabu. Wanakabiliwa na miamala isiyo ya kibinadamu na ya kibaguzi.
Waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu tabia ya Israel isiyo ya kibinadamu na ya dharau dhidi ya wanawake na wasichana wa Kipalestina. Televisheni ya Al-Jazeera ilifichua hivi karibuni, ikimnukuu raia mmoja wa Palestina aliyezingirwa katika jengo la matabibu la Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza, kwamba wanajeshi wa Israel waliwabaka wanawake kadhaa wa Kipalestina katika eneo hilo na kisha kuwaua kinyama.
Ripoti za kuaminika kuhusu kunyongwa wanawake na watoto wa Kipalestina na pia kukamatwa kwa lazima na kuhamishiwa vizuizini katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zimeandikwa na kuchapishwa na waandishi wa habari wa kimataifa.
Unyanyasaji dhidi ya wanawake pia umeongezeka katika nchi nyingine kama vile Afghanistan. Tarannum Saeedi, mkuu wa Mtandao wa Ushiriki wa Kisiasa wa Wanawake wa Afghanistan, anasema: “Wanawake wa Afghanistan wanaadhimisha tarehe 25 Novemba mwaka huu huku wakikabiliwa na ongezeko la unyanyasaji, udhalilishaji wa kijamii na dhuluma za kimfumo.
Wanawake wa Ulaya na Marekani pia wako chini ya unyanyasaji na ukosefu wa usawa, hivi kwamba wengi nchini Ufaransa na Italia walifanya maandamano siku chache zilizopita kulalamikia suala hilo. Waandamanaji katika miji ya Rome, Paris, Marseille na Lille walipinga aina zote za ukatili dhidi ya wanawake, zikiwemo za kingono, kimwili, kisaikolojia na kiuchumi.
Huko Marekani, wanawake na wasichana, haswa wahamiaji na watu kutoka Amerika ya Latini, hupitia hali ngumu. Ripoti zinaonyesha kwamba kwa wastani mwanamke mmoja kati ya kila watatu Amerika ya Latini ni mwathirika wa vitendo vya mabavu nyumbani. Wakati huo huo, mwanamke mmoja kati ya kila wawili amepitia vitendo hivyo wakati fulani katika maisha yake ya ndoa.
Kwa hiyo, unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana bado ni mojawapo ya kesi zilizoenea zaidi za ukiukwaji wa haki za binadamu duniani, na kimya kuhusu suala hilo na kutoshughulikiwa vilivyo kisheria ni jambo ambalo limefanya mwenendo huu uendelee bila kusita.