Siku 16 za moto zapeleka kilio Azam

Dar es Salaam. Kipigo cha mikwaju ya penalti 4-2 ambacho Azam FC imekipata nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex jana, kimeiweka timu hiyo kwenye uwezekano finyu wa kuondoka na taji msimu huu.

Baada ya kutopata taji na jana kutolewa na Mbeya City kwenye Kombe la Shirikisho la Azam baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za mchezo, matumaini pekee ya Azam FC kupata Kombe yamebakia katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo hata hivyo ina mfupa mgumu kwani ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 45, ikizidiwa kwa pointi tisa na Simba iliyo katika nafasi ya tatu na imeachwa na kinara Yanga kwa pointi 13.

Kichapo cha jana kutoka kwa Mbeya City, kimekamilisha siku 16 za moto ambazo kocha Rachid Taoussi na kikosi chake cha Azam FC wamepitia ambazo zinaweza kutafsirika kama zimeweka rehani ndoto za timu hiyo kuondoka na taji msimu huu.

Katika kipindi hicho cha siku 16, Azam FC imecheza mechi nne mfululizo za mashindano tofauti bila kupata ushindi na zote ikiambulia sare katika dakika 90 za mechi.

Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Aza Complex, Februari 15, mwaka huu, mechi iliyofuata, Azam FC ililazimishwa sare tasa na Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Februari 19.

Februari 24 ikatoka sare ya mabao 2-2 na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Februari 27 ikalazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Namungo FC kabla ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City kisha kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-2.

Ofisa habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema kuwa kutolewa kwao na Mbeya City kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB, kumewaumiza.

“Nikisema Mbeya City wabovu nitakuwa sina adabu na mpira nawapa hongera kwa ushindi wa leo. Kwa timu yangu Azam Fc tumeingia uwanjani tukiwa chaguo la kwanza lakini tumeishia kuwa timu ya pili kwa sababu hatukucheza tulivyopaswa kucheza na kama kuna mtu wa kuwajibika leo basi ni sisi viongozi wote, benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla si wengine.

“Tunaomba radhi kwa matokeo mabovu leo tumeshindwa kufika hatua muhimu za mashindano haya ambayo kwa miaka miwili mfululizo iliyopita tumecheza hatua ya fainali tena tukiwa bora sana.

“Kwa haya matokeo ya leo (jana) ni dhahiri kwamba tuonane mwakani we need to Up our Game,” alisema Ibwe.