
MSHAMBULIAJI Kinda wa Trident FC ya Zambia, Mourice Sichone amesema ujumbe aliouchapisha kwenye jezi yake unamlenga mama yake mzazi ambaye yuko hospitali akiuguza majeraha ya ajali aliyopata wiki iliyopita.
Kinda huyo (18) alisajiliwa dirisha dogo akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini humo akicheza mechi 12 na kufunga mabao manne na asisti tano.
Msimu uliopita Trident ilishuka daraja baada ya kumaliza mkiani na pointi 26 na kushiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sichone alisema sababu ya kufanya hivyo ni kumfariji mama yake mzazi ambaye ndiye mtu anayemsapoti kwenye maisha yake ya soka.
“Mama yangu anaumwa sana, alipata ajali na ndiye mtu pekee ambaye anapenda sana na kunisapoti kitu ninachokifanya na siku zote kabla sijacheza mechi lazima anipigie simu na kuniombea, nampenda sana ndiyo maana nilipofunga bao la kuipa timu yangu sare 1-1 niliutoa ujumbe ule,” alisema Sichone ambaye hilo ndiyo bao lake pekee katika mechi tatu alizocheza msimu huu.