
Dar es Salaam. Rais Donald Trump na Rais mstaafu Joe Biden wameagana kwa siasa za piga nikupige, huku Biden akimsamehe mwanawe Hunter Biden kwa makosa ya jinai na Trump akiwasamehe wafuasi wake 1,500 waliovamia Bunge 2021.
Ni siasa za ‘piga nikupige’ ambapo baada ya Trump kuapishwa alisema “enzi ya dhahabu ya Marekani inaanza,” huku akitilia mkazo falsafa yake ya kuifanya Marekani kuwa taifa kubwa tena (MAGA).
Kiongozi huyo kutoka chama cha Republican alisema hayo katika hotuba yake ya kwanza kama Rais wa 47 wa Marekani.
Trump, ambaye alimshinda Makamu wa Rais kutoka chama cha Democratic, Kamala Harris Novemba 5, sasa, akiwa na umri wa miaka 78, ndiye mkuu wa nchi mzee zaidi wa Marekani kuwahi kuapishwa.
Katika siku yake ya kwanza, Trump alibatilisha amri 78 na vitendo vilivyotiwa saini na utawala wa Biden.
Trump pia alitia saini amri ya Serikali kurejesha uhuru wa kusema na kuzuia udhibiti wa uhuru wa kujieleza na moja kumaliza ‘silaha za serikali’ dhidi ya wapinzani wa kisiasa wa utawala uliopita’.
Mtoto wa Joe Biden
Trump kama vile analipa kisasi kwa ‘piga nikupige’, amesaini amri ya kuondoa ulinzi kwa maofisa 51 wa ujasusi walioonekana kutumika kumkinga na kesi ya jinai mtoto wa Biden, Hunter Biden.
Maofisa hao walitia saini barua wakisema kwamba barua pepe kutoka kwenye kompyuta ndogo ya Hunter Biden zilikuwa na “alama zote za kawaida za operesheni ya habari ya Urusi” na ile ya raia wake wa zamani mshauri wa usalama John Bolton.
Licha ya maofisa hao ambao wengi wamestaafu, lakini agizo hilo linapendekeza kwamba Trump anakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
“Wanapaswa kufunguliwa mashtaka kwa kile walichokifanya,” Trump alisema kuhusu maofisa 51 waliotia saini barua hiyo.
Trump asamehe wafuasi wake
Piga nikupige iliendelea kwa Trump kutoa msamaha kwa wafuasi wake 1,500 waliokuwa na kesi ya kuvamia Bunge Januari 6, 2021, ikiwamo kuzifuta kesi zote zilizowahusu.
Wafuasi hao walivunja sheria kwa kuvamia ndani ya Bunge la Marekani wakati linajadili kuthibitishwa kwa kura za wajumbe za matokeo ya uchaguzi wa rais ambapo mshindi alikuwa Biden.
Waandamanaji hao waliharibu baadhi ya sehemu ya jengo hilo, ikiwemo madirisha na milango, wakidai mgombea wao Trump ameibiwa kura na Biden.
Pia, Baraza la Seneti la Marekani lilianza mchakato wa kusikiliza mashitaka dhidi ya Trump akituhumiwa kuchochea vurugu hizo.
Mbali na msamaha huo, pia alimuelekeza mwanasheria mkuu wa Serikali kufuta kesi za jinai 450 dhidi ya wafuasi hao waliovamia Bunge.
Msamaha wa Biden
Kabla ya kukabidhi madaraka kwa Trump, Rais Biden alitumia uwezo wake wa kiutendaji kuwalinda watu alioona walengwa wa Trump, wakiwemo watu watano wa familia yake Biden na wengine Liz Cheney, Anthony S. Fauci na Mark A. Milley.
Rais Biden alitoa msamaha katika saa zake za mwisho ofisini Jumatatu ya Januari 20,2025 ili kuwalinda watu wa familia yake na watu wengine mashuhuri kutokana na kampeni iliyoahidiwa ya “kulipiza” na mrithi wake Trump.
Katika juhudi zisizo za kawaida za rais anayeondoka madarakani kuzuia mashtaka ya kisiasa ya rais anayekuja, Biden aliwasamehe watu watano wa familia yake, wakiwemo kaka zake James B. Biden na Francis W. Biden, pamoja na wengine waliolengwa na Jenerali Mark A. Milley, Dk Anthony S. Fauci na Liz Cheney.
“Ninaamini katika utawala wa sheria, na nina matumaini kwamba nguvu za taasisi zetu za kisheria hatimaye zitashinda siasa,” alisema Biden na kuongeza: ” Uchunguzi usio na msingi na unaochochewa kisiasa huharibu maisha, usalama na usalama wa kifedha wa watu wanaolengwa na familia zao.
“Hata wakati watu hawajafanya chochote kibaya na kwa kweli wamefanya jambo sahihi na mwishowe wataondolewa hatia, ukweli wa kuchunguzwa au kufunguliwa mashtaka unaweza kuharibu sifa na fedha bila kifani,” aliongeza.
Msamaha kwa mwanawe
Biden mwaka jana baada ya Trump kushinda uchaguzi, alitoa msamaha kwa mtoto wake Hunter, ambaye angehukumiwa kwa makosa ya kumiliki silaha na kodi na huenda angehukumiwa kifungo cha miaka kadhaa jela.
“Tuhuma hizi za kesi yake zililetwa baada tu ya wapinzani wangu wa kisiasa katika Bunge kuwachochea kunishambulia na kupinga kuchaguliwa kwangu,” alisema Biden.
Msamaha huo ulipingwa na Rais mteule kwa wakati huo, Trump akisema hatua hiyo ni kutumia sheria vibaya.
Hunter Biden alikutwa na makosa ya jinai matatu kwa kununua bunduki mwaka 2018. Waendesha mashtaka walisema alidanganya katika fomu ya Serikali kuu kuwa hatumii kinyume cha sheria au hana uraibu wa dawa za kulevya.
Hatua za kiuchumi
Pia, Trump amesaini amri ya ongezeko la ushuru wa forodha wa asilimia 25 kwa bidhaa za China, Canada na Mexico, huku akitoa muda kwa Canada na Mexico kwamba ushuru utaanza kutozwa Februari Mosi. China hakutaja tarehe.
Wakati wa kampeni, Trump alitangaza iwapo atashinda urais ataweka ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa za China, Canada na Mexico.
Alisema hatua zake za kwanza za kiuchumi baada ya kuapishwa kwake zitakuwa kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazotoka China, lakini pia kutoka Canada na Mexico. “Januari 20, kama moja ya maagizo yangu ya kwanza ya kama Rais, nitatia saini hati zote muhimu za kutoza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote zinazoingia Merikani kutoka Mexico na Canada,” aliandika kwenye ukurasa wake wa X.
“Ushuru huu utaendelea kutumika hadi dawa za kulevya, hasa ‘fentanyl’, na wahamiaji haramu wote wakomeshwe kuvamia nchi yetu,” aliongeza.
Ongezeko la ushuru wa forodha, ambalo mara nyingi alilielezea kama “tamko analopenda zaidi” wakati wa kampeni yake, ni moja ya ufunguo wa sera ya baadaye ya kiuchumi ya kiongozi huyo
ambaye haogopi kuanzisha tena vita vya biashara, hasa na China, vilivyoanza wakati wa muhula wake wa kwanza. Kuhusu China, aliahidi ushuru wa forodha wa hadi asilimia 60 kwa baadhi ya bidhaa, au hata asilimia 200 kwa uagizaji wa magari kutoka Mexico.
Sheria za Marekani zinampa Rais uwezo wa kutekeleza ushuru wa forodha kwa amri. Trump katika muhula wake wa kwanza aliweza kutumia sheria hiyo kwenye chuma na alumini kutoka China na Ulaya.