Dar es Salaam. Ushawahi kujiuliza katika wimbo wa Mwana FA ‘Bado Nipo Nipo’ ni sauti ya mrembo yupi anayeuliza “Mwana FA unaoa lini?”, basi yule ni Flaviana Matata, Mwanamitindo wa kimataifa kutokea nchini Tanzania.
Huyu ni mshindi wa Miss Universe Tanzania 2007, tangu wakati huo Flaviana aliendelea kufanya vizuri kimataifa upande wa mitindo na kubwa zaidi ni utamaduni wake wa kurudisha katika jamii kile ambacho anakipata.

Ukubwa wa kazi yake umepelekea Flaviana kuandikwa kwenye majarida makubwa na maarufu duniani kama Forbes Africa, French Magazine, Schon, Dazed & Confused, Glass Magazine, L’officiel, ID Magazine, Marie Claire n.k.
Mwaka 2013 Flaviana alitajwa na Forbes Africa katika orodha ya Wanamitindo wanaolipwa fedha nyingi zaidi, huku mwaka 2017 akitajwa na Okay.com kuwa ni miongoni mwa wanawake 100 bora Afrika.
Kazi yake ambayo mara nyingi aliifanya New York, Marekani, imemkutanisha na watu maarufu duniani kama Nicki Minaj, Mary J. Blige, Jay Z, Beyonce, Lady Gaga na Russel Simmons ambaye ni mwanzilishi wa Def Jam Recordings.
Aprili 2019 Flaviana alitokea kwenye tangazo la bidhaa za vipodozi vya Rihanna, Fenty Beauty, kampuni iliyozinduliwa mwaka 2017 kwa kushirikiana na kampuni ya bidhaa za kifahari, LVMH.

Rihanna ambaye ni mwanamuziki wa kike wa pili duniani kwa utajiri akiwa na ukwasi wa Dola1.4 bilioni, kamfuata (follow) Flaviana katika mtandao wa Instagram, Flaviana anatajwa ndiye Mtanzania pekee aliyepata bahati hiyo.
Flaviana amefanikiwa kupata tuzo kama Arise Fashion Magazine Awards (2011), Nigeria Next Super Model Awards (2012), Africa Diaspora Awards (2012), Swahili Fashion Week Awards (2012), Malkia wa Nguvu Awards (206), Global Woman Gala (2018) n.k.
Hakuna ubishi kati ya wanawake kutoka kiwanda cha burudani na mitindo Bongo wanaopaswa kupewa maua yao kwa sasa, ni Flaviana Matata kutokana na jitihada zake za miaka mingi kuchangia elimu hasa kwa watoto wa kike nchini Tanzania.
Mwimbaji wa RnB, Pop na Soul, Whitney Houston kupitia wimbo wake, Greatest Love of All (1986) anaamini kuwa watoto ndio wenye mazuri yetu ya baadaye, hivyo tuwafundishe vizuri na kuwaacha waongoze njia kwa kuwaonyesha mazuri yaliyopo ndani yao.
“Everybody searching for a hero, people need someone to look up to (Kila mtu anamtafuta shujaa, watu wanahitaji mtu wa kumtazama kama mfano)” Whitney katika wimbo huo uliotoka chini ya Arista Records.
Imepita miaka 39 tangu Whitney Houston kuimba wimbo huo ambao awali ulirekodiwa na George Benson mwaka 1977, maneno hayo yanaishi katika kile anachofanya Flaviana kupitia taasisi yake, Flaviana Matata Foundation (FMF).
“Ikiwa tunaamini kweli kwamba kila msichana katika kila kona ya ulimwengu anastahili kupata elimu kama vile binti zetu na wajukuu zetu, basi tunahitaji kuimarisha kujitolea kwetu kwa juhudi,” alisema Michelle Obama, mke wa Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama.

Maneno hayo yapo tovuti ya Flaviana Matata Foundation (FMF) iliyozinduliwa Juni 2011 ikiwa na lengo la kuanzisha mfuko wa kusaidia elimu ya watoto waishio katika mazingira magumu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Mtoto ni kama wa kwetu tunamuhudumia kila kitu, nimeweka fedha nyingi sana, hujasikia nimefanya fundrise, kuna watu wananisadia sikatai, mtu aliyeko kwenye taasisi yangu anajua ni kiasi gani nimeweka kutoka mfukoni mwangu na sijilipi!,” anasema Flaviana.
Mwaka juzi FMF ilikabidhi mradi wa matundu ya vyoo 24 katika shule ya Mazinge wilayani Shinyanga, walishakabidhi nyumba kwa walimu shule Msinune wilayani Chalinze na kwingineko nchini, pia wamekuwa wakilipia wanafuzi ada, vifaa n.k.
Muhubiri Joyce Meyer katika kitabu chake, Love Revolution (1987) anasema kila asubuhi anapokaa na kunywa kahawa yake, ghafla anafikiria watu milioni 963 duniani wana njaa, zaidi ya watu bilioni 1 wana kipato cha chini ya Dola1 kwa siku.
Watoto 30,000 watafariki hii leo sababu ya umaskini, wanafariki katika baadhi ya vijiji maskini zaidi duniani wakiwa mbali kufikiriwa na ulimwengu. Hiyo ni sawa na watoto 210,000 hufariki kila wiki, sawa na watoto milioni 11 kila mwaka na wengi wao wako chini ya umri wa miaka mitano!.

Meyer anasema kati ya watoto bilioni 2.2 walioko duniani, milioni 640 hawana makazi, milioni 400 hawapati maji safi ya kunywa na milioni 270 hawapati huduma zozote za matibabu. Kwa muktadha huo, juhudi za watu kama Flaviana kuwapatia watoto elimu ni za kupongezwa na kuungwa mkono maana elimu ndio mkombozi wao.
Kama alivyosema Jessica Cox katika kitabu chake, Disarm Your Limits (2015) kuwa huhitaji kuwa na mikono ili uwainue watu kutoka chini bali unahitaji moyo wa upendo wa dhati kwa kuwaonesha wanaweza kufanya mambo makubwa, ndivyo anavyofanya Flaviana Matata.
Ikumbukwe Jessica anashikilia rekodi ya dunia ya Guinness kama mtu wa kwanza duniani asiye na mikono aliyepewa leseni ya kurusha ndege, hivyo alirusha na kuongoza ndege kwa kutumia miguu yake.