Si UN na WHO pekee, hata waitifaki wa Israel wapinga na kulaani uamuzi wa kuipiga marufuku UNRWA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amemwandikia barua waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni akisema, ametiwa wasiwasi mkubwa sana na uamuzi wa utawala huo wa kupitisha sheria ya kupiga marufuku shughuli za Shirika la UN la misaada kwa wakimbizi Wapalestina UNRWA na kusisitiza kuwa uamuzi huo haukubaliki.

“Hakuna mbadala wa UNRWA,” amesisitiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika barua yake.

Guterres amebainisha kuwa utekelezwaji wa sheria zilizopitishwa na Israel unaweza kuwa na matokeo mabaya kwa wakimbizi wa Kipalestina katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina, jambo ambalo halikubaliki.

Amefafanua kwa kusema: “ninatoa wito kwa Israel kuchukua hatua zinazoendana na wajibu wake kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na wajibu wake mwingine chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa za kibinadamu na zile zinazohusu haki na kinga za Umoja wa Mataifa. Sheria za kitaifa haziwezi kubadilisha majukumu hayo.”

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus yeye amesema UNRWA imekuwa “njia ya maisha isiyo na mbadala” kwa Wapalestina kwa muda wa miongo saba sasa na kusisitiza kuwa uamuzi uliochukuliwa na Israel wa kulipiga marufuku shirika hilo “hauvumiliki”.

Amekumbusha kuwa UNRWA iliundwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba uamuzi wa bunge la Israel wa kuzuia UNRWA kufanya kazi yake ya kuokoa maisha na kulinda afya za mamilioni ya Wapalestina utakuwa na matokeo mabaya.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan “imelaani vikali” hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni na kuielezea kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na wajibu wake ukiwa ni utawala unaokalia ardhi kwa mabavu.

UNRWA yenyewe kupitia mkuu wake Philippe Lazzarini, China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Canada, Ireland, Norway, Slovenia, Uhispania, Australia, Japan na Korea Kusini, zimekosoa na kulaani uamuzi wa Israel na kuutaka utawala huo ghasibu uangalie upya uamuzi wake huo.

Bunge la utawala haramu wa Kizayuni, Knesset limepitisha mswada unaoizuia UNRWA kuendelea na operesheni zake katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Baitul Muqaaddas Mashariki (Jerusalem Mashariki) na Ukanda wa Ghaza.

Mswada huo unapiga marufuku shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina kufanya “shughuli yoyote” au kutoa huduma yoyote ndani ya ‘Israel’…/