Si bure, Tanzania Prisons kuna mkono wa mtu

ACHANA na matokeo ya Azam FC kuondoshwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kufungwa na Mbeya City, hali imezidi kuwa mbaya kwa Tanzania Prisons ikiendelea kuyumba ikiwa ni kati ya timu nne za Ligi Kuu Bara zilizong’olewa katika michuano ya Shirikisho.

Prisons ilitolewa na Bigman (zamani Mwadui) iliyopo Ligi ya Championship kwa mikwaju ya penalti kama ilivyokuwa kwa Azam na kuungana na KenGold na Dodoma Jiji zilizotolewa katika michuano hiyo hadi sasa ikiwa katika hatua ya 32 Bora kusaka timu za 16 Bora.

Ikiwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na wenyeji wa mchezo huo, Prisons iliyokuwa wenyeji walijikuta wakilala kwa penalti 2-3 mbele ya Bigman baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.

Huo unakuwa mchezo wa sita mfululizo kwa maafande hao kucheza bila kuonja ushindi chini ya Kocha Aman Josiah aliyekabidhiwa mikoba hivi karibuni akiziba nafasi ya Mbwana Makatta.

Katika michezo saba aliyosimamia Josiah ameshinda mmoja dhidi ya Mashujaa 2-1, akitoa sare moja na kupoteza minne na kuwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 18.

Matokeo hayo yanaendelea kuiweka kwenye presha kubwa ya kukwepa kushuka daraja, lakini ikiwa ni mwenendo usiyoridhisha na kuonekana kupiga hatua moja mbele na 10 nyuma tangu kuondoka kwa Makata.

Baada ya kupoteza mchezo huo, timu hiyo inatarajia kurejea uwanjani keshokutwa Alhamisi kuwavaa Azam ambao nao hawapata ushindi katika michezo minne mfululizo ikiwa ni sare tatu na kupoteza mmoja.

Mchambuzi wa soka jijini Mbeya, James Shija alisema matokeo ya Kombe la FA kwa timu hiyo yanaweza kuwaumiza au kuwapa nafasi kujipanga kwa mechi za Ligi Kuu.

“Kocha atakuwa na wakati mgumu kuwaandaa vijana kisaikolojia, unapofungwa na timu ya chini kwenye mashindano wakati huo timu haina matokeo mazuri inaweza kuathiri kiakili wachezaji.”

“Lakini Prisons kutupwa nje inaweza kuwapa nafasi ya kuweka akili kwenye mechi za Ligi Kuu kwakuwa hawako salama, wanapambana kubaki Ligi Kuu,”  alisema Shija.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi ya Muungano wa Tanzania, imekuwa na misimu kadhaa mibaya kwa siku za karibuni ni kunusurika kushuka daraja kupitia mechi za play-off na safari hii hali imeonekana kuwa mbaya, hasa baada ya kuondolewa kwa baadhi ya mastaa wakongwe.

Wachezaji hao kama Salum Kimenya, Jumanne Elfadhili na walio majeruhi Samson Mwamanda na Jeremiah Juma, huku kina Ibrahim Abraham, kipa Yona Amosi na Zabona Mayomba kutimkia Pamba Jiji kumeifanya Prisons kuyumba, japo kocha Josiah alinukuliwa bado anaamini waliopo wataibeba.