
KOCHA wa zamani wa Yanga, Raoul Shungu ameitahadharisha timu hiyo akiwaambia wawe makini na kiungo wa mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu kutokana na uwezo wake wa kubadilisha mchezo aliokuwa nao DR Congo.
Mpanzu aliyetua Simba dirisha dogo amekuwa akipata nafasi katika kikosi hicho tangu alipoanza kukitumikia huku akiweka rekodi ya kuhusika katika mabao manne akifunga mawili na asisti mbili.
Katika mechi 10 za mwisho ilizocheza Simba, Mpanzu amekuwa akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza hii ikionyesha kocha Fadlu Davids, amevutiwa na kiwango alichonacho licha ya kutokufunga mabao mengi.
Simba inashika nafasi ya pili, ikiwa imecheza mechi 21 na kuvuna alama 54 na kufikisha jumla ya mabao 46, huku Mpanzu akifunga mawili na kuasisti mawili vilevile.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shungu aliyewahi kumnoa Mpanzu akiwa AS Vita ya DR Congo, alisema Yanga inatakiwa kujitahadharisha na nyota huyo, kwani ana uwezo mkubwa wa kubadili mchezo.
Alisema, kama wachezaji wa Yanga watakuwa wavivu wa kukimbia kidogo na kutumia nguvu atawasumbua katika mechi ya leo ya Kariakoo Dabi.
“Mpanzu ni mchezaji ambaye timu yake inaweza kuwa katika wakati mgumu uwanjani, lakini akapambana kuirudisha mchezoni. Pia anajua kufunga kwa kujaribu kutoka mbali ni mchezaji mbunifu sana uwanjani, hivyo beki atakayekabana naye atakuwa na kazi,” alisema Shungu.
Katika nafasi anayocheza Mpanzu yuko pia Awesu Awesu, Edwin Balua, Ladack Chasambi, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis, ambaye naye amekuwa na uwezo wa kuamua mechi.
Kwa rekodi alizonazo tangu atue Msimbazi, kuna kila dalili kwamba Mpanzu leo akaanzishwa kikosi cha kwanza na hivyo mabeki wa Yanga wanaokutana naye kwa mara ya kwanza kuwa na kazi ya kumzuia asiwaletee madhara, ikikumbukwa pia kikosi hicho pia kina Kibu aliyefunga mara mbili katika misimu miwili iliyopita.