Shughuli mbalimbali zasimimama kwa muda Arusha

Arusha. Wakati wananchi wakijitokeza kupiga kura katika maeneo mbalimbali kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, baadhi ya shughuli ikiwemo wafanyabiashara kufunga maduka yao, kupisha upigaji kura unaoendelea kote nchini.

Mwananchi imeshuhudia sehemu mbalimbali za biashara ikiwemo maduka mengi kuchelewa kufunguliwa.

Tofauti na siku zingine maduka hayo hufunguliwa mapema, lakini leo Jumatano Novemba 27, 2024 hali imeonekana kuwa tofauti na siku zingine ambapo maduka mengi yalianza kufunguliwa.

Maduka mengi hususani yaliyopo Barabara ya Uhuru na maeneo mengine hadi saa tatu asubuhi yalikuwa hayajafunguliwa ambapo baadhi yao yameanza kufunguliwa saa nne.

Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura baadhi ya wananchi wamelalamikia kutokuona majina yao kwenye orodha.

Aidha changamoto nyingine waliyolalamikia ni majina yaliyobandikwa kutokuwa katika mtiririko wa silabi hali inayowapa ugumu kutafuta majina yao.

“Mimi nilijiandikisha hapa katika Kituo cha Shule ya Sekondari Kaloleni ila jina langu halipo kwenye orodha pale. Changamoto nyingine ni majina kutokuwa kwenye mtiririko, hiyvo inatuwia ugumu kupata majina yetu kwa wakati,” amesema Anne Mollel.

Endelea kufuatilia Mwananchi.