Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetangaza kukamilika kwa mradi wa Samia Housing Scheme, awamu ya kwanza uliopo eneo la Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam ambapo wanunuzi wa awamu hiyo wanatarajiwa kukabidhiwa rasmi nyumba zao kuanzia mwezi huu hadi katikati ya mwezi ujao.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, amesema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukamilika kwa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea miradi muhimu ya kimkakati inayotekelezwa na shirika hilo, ikiwemo Kawe 711, Samia Housing awamu ya kwanza, Morocco Square, pamoja na mradi wa GPR ambao ulikuwa umesimama kwa takribani miaka minane sasa.
Akifafanua zaidi kuhusu mikakati ya maendeleo ya shirika hilo, Abdallah amesema NHC inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati yenye lengo la kuboresha miji kwa kuvunja majengo chakavu na kujenga mapya, kuanzisha vitovu vya miji (satellite cities), kuendeleza miliki kwa mfumo wa ubia, na kujenga nyumba za gharama mbalimbali ili kila Mtanzania aweze kuishi katika makazi bora na ya kisasa.
Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa tayari NHC imeanza kutekeleza mpango mkubwa wa kulibadilisha kabisa eneo la Kariakoo ambalo kwa muda mrefu limekuwa na majengo chakavu, kwa kujenga majengo ya kisasa yatakayoanzia ghorofa 10 kwenda juu, kulingana na mahitaji ya sasa ya makazi na biashara.
“Hakutakuwa tena na jengo chakavu la NHC katika Kariakoo ndani ya miaka mitatu. Tayari tumeanza na miradi 16 ambapo majengo ya zamani yamevunjwa na ujenzi mpya unaendelea. Kwa ujumla, majengo 64 yataondolewa na kujengwa upya kama sehemu ya mageuzi haya ya kimkakati,” amesema Abdallah.
#azamnewsupdates
✍Esterbella Malisa
Mhariri| @official_jennifersumi