Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesimamisha kwa muda shughuli zake katika jimbo la Djibo kaskazini mwa Burkina Faso kutokana na masuala ya usalama.
Shirika la MSF limechukua uamuzi huo baada ya vituo vya afya na vya kusambaza maji kushambuliwa mara kwa mara.
Moussa Ousman Meneja Mipango wa kundi hilo la masuala ya kibinadamu amesema kuwa shirika hilo linahitaji usalama wa kutosha ili kuruhusu timu ya wafanyakazi wake kuendelea na shughuli zao za kutoa misaada kwa jamii zilizoathiriwa na ukosefu wa usalama na machafuko.
Shirika hilo lisilo la kiserikali limesisitiza kuwa linatoa kipaumbele kwa usalama wa wafanyakazi wake na kuwaruhusu kutathmini upya hali ya kazi kwa kuzingatia ugumu wa mazingira ya kazi unaoongezeka katika kutoa misaada ya matibabu kwa jamii mbalimbali.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) linaendelea kutoa misaada ya kibinadamu katika majimbo kadhaa ya Burkina Faso ambapo hadi sasa limehudumia wagonjwa 348,477. Zaidi ya wagonjwa 3,120 wa afya ya akili wametibiwa, na karibu lita milioni 72 za maji zimesambazwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu huko Burkina Faso.