
Katika kuhakikisha michezo ya jadi ikiwamo ngoma za asili, mchezo wa rede na mingine inachezwa na kuendelezwa, Mkoa wa Shinyanga umeandaa tamasha la michezo hiyo litakalofanyika Aprili 12, mwaka huu.
Tamasha hilo pia linalenga kupata wachezaji watakaounda timu ya mkoa kwa ajili ya kuwakilisha katika mashindano ya taifa ya mchezo wa jadi yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu jijini Dodoma.
Akizungumzia mipango ya tamasha hilo, Mratibu wa Chama Michezo ya jadi Taifa (Chamijata), Abubakary Kyaibamba amewataka viongozi wa chama hicho mkoani Shinyanga kufufua michezo hiyo na kuhamasisha ichezwe katika jamii kwani imesahaulika.
Kyaibamba amesema tamasha hilo litasaidia kukuza michezo hiyo na kuipa hamasa huku wakitarajia kupata wawakilishi bora kwa ajili ya kuuendeleza mchezo huo.
“Utafiti ufanyike kwa michezo ya jadi kuifufua na kuiibua upya ili itambulike katika ngazi ya kimataifa hasa tukianza na mbina (ngoma za jadi), bao na rede kwa wanawake ipelekwe ngazi ya kimataifa,” amesema Kyaibamba.
Mwenyekiti wa Chama cha Michezo ya Jadi Mkoa wa Shinyanga, Isaya Meru amesema katika mikoa ya Kanda ya Ziwa mchezo wa ngoma za jadi ndiyo unafahamika na umejizolea umaarufu huku akipendekeza uwe kati ya michezo itakayoendelezwa na kujumuishwa katika mashindano ya kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Aprili 26, mwaka huu.
“Mchezo wa Mbina (ngoma za jadi) uwe ni moja kati ya michezo itakayopelekwa katika mashindano yatakayofanyika Dodoma na hatimaye kushindana kimataifa kwa sababu unapendwa na jamii nyingi na kila kabila lina ngoma yake ya asili kwahiyo itaongeza hamasa na kuleta ushindani,” amesema Meru.
Mmoja wa wazazi kutoka kata ya Ngokolo mjini Shinyanga, Amina Selemani amesema kuwa michezo ya jadi itasaidia vijana kuwa na ufahamu kuhusu tamaduni za Kitanzania kwa sababu wengi wao wamemezwa na utandawazi kwa kuiga kuiga tamaduni kutoka mataifa ya nje ambazo zinaharibu maadili ya Kitanzania.
“Tamasha la michezo ya jadi litafungua akili za vijana wengi ambao hawajui tamaduni za Kitanzania kwa kukumbwa na utandawazi ikiwa na kuiga tamaduni za nchi za magharibi na kusahau jadi yetu,” amesema Amina.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, Janeth Mushi amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na chama cha mchezo huo kitaifa (Chamijata) atahakikisha yanafanyiwa kazi na kuhakikisha tamasha hilo la mkoa linaenda kama ilivyopangwa.