Shinikizo la damu laongoza kusababisha vifo, wataalamu waonya

Dar es Salaam. Licha ya dalili za ugonjwa wa shinikizo la juu la damu kujulikana, wataalamu wa afya wamesema kwa baadhi ya hawapati  dalili za moja kwa moja kuonyesha shinikizo lipo juu, isipokuwa kwa njia ya vipimo.

Kwa mujibu wa wataalamu, ni vigumu kubaini ikiwa shinikizo la damu liko juu kulingana na jinsi mtu anavyohisi.

“Mara nyingi watu hufikiri kuwa maumivu ya kichwa, kutokwa na damu puani, kizunguzungu, kuhisi uchovu na dalili nyingine za jumla hutokana na shinikizo la juu la damu. Lakini dalili hizo hazithibitishi kuwa na tatizo hilo, kwani unaweza kuwa nazo na shinikizo lako la damu ni la kawaida,” amesema Dk Tasekeen Khan, Ofisa wa kitengo cha magonjwa ya moyo na mishipa wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hata hivyo, amesema ikiwa shinikizo lako la juu la damu limesababisha matatizo, kama vile shambulio la moyo, moyo kushindwa kufanya kazi, au kiharusi, unaweza kuwa na dalili kama vile maumivu ya kifua, kuishiwa pumzi, maumivu ya kichwa, kuchanganyikiwa au kutatizika kuzungumza, uoni hafifu na udhaifu au kupooza kwa upande mmoja wa mwili au uso.

Dk Tasekeen ameeleza kuwa tatizo hilo ni sababu kuu ya kifo cha mapema duniani kote, huku akifafanua kwa kina kwa nini shinikizo la juu la damu linatambulika kama muuaji wa kimyakimya.

“Inaitwa ‘silent killer’ kwa sababu huzioni kabisa dalili na ndiyo maana kwa sasa tatizo hili linaathiri mtu mmoja kati ya watu wazima watatu duniani na kati ya watu watano wenye shinikizo la juu la damu ni mmoja pekee anayeweza kudhibiti hali hiyo kwa matibabu,” amesema Dk Tasekeen.

Daktari mshauri mwandamizi magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Harun Nyagori amesema kuna umuhimu kwa jamii kuchunguza afya kwani wengi wenye shinikizo la damu hawafahamu hali zao mapema.

“Tatizo la shinikizo la damu linaweza kukupata na isionyeshe dalili yoyote kwa walio wengi, tatizo ni kubwa kwa kuwa wengi hawatambui hali zao, wanapogundulika tayari madhara ni makubwa mfano tayari ana kisukari, mshtuko wa moyo na matatizo ya figo kushindwa kufanya kazi,” amesema.

Profesa Nyagori amesema wengi wa wagonjwa kutotumia dawa kwa maelekezo sahihi na wengine kusitisha kabla ya kupewa maelekezo na wataalamu ni changamoto kubwa.

Ametaja wengi kutofuata maelekezo ya chakula kama kuongeza chumvi mezani, utumiaji kupitiliza wa pombe kali, msongo wa mawazo na kukataa kufanya mazoezi rahisi wanayoelekezwa.

“Wengine ni kutoamini kuwa anaumwa au shinikizo la damu linaweza likamletea madhara makubwa na wengine kuamini imani za kishirikina au potofu na kukataa kupata uchunguzi na matibabu sahihi,” amesema Nyagori.

Ukubwa wa tatizo

Ripoti ya utoaji wa huduma za kibingwa kwenye hospitali 184 ngazi ya halmashauri kupitia mpango wa madaktari bingwa wa Samia, iliyofanyika Mei mpaka Julai mwaka 2024, ilionyesha asilimia 34 ya waliojitokeza walikuwa na shinikizo la juu la damu.

Jumla ya wagonjwa 70,000 walioonwa na kambi hiyo kati ya 22,057 wa magonjwa ya ndani, shinikizo la juu la damu liliongoza kwa wagonjwa 7,529 sawa na asilimia 34 ikifuatiwa na matatizo ya mfumo wa chakula wagonjwa 4,158 sawa na asilimia 9.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge  ameliambia Mwananchi kuwa wagonjwa wanaofuata huduma katika vituo vya afya idadi ya wenye shinikizo ni kubwa ikilinganishwa na magonjwa mengine katika jamii.

“Tunapoenda kwenye jamii tunaomba takwimu kama hizo, kwa JKCI hapa asilimia 30 ya wagonjwa tunaowaona wana shinikizo la juu la damu na kwenye kambi tukiwafuata mitaani tunawapata asilimia 25,” amesema akishauri jamii kubadili mtindo wa maisha.

Shinikizo la juu la damu ni tatizo la kiafya linaloongezeka duniani na kuwa sababu kuu za vifo na ulemavu, ikiwa ni pamoja na mshtuko wa moyo, kiharusi na kufeli kwa figo.

Kwa mujibu wa ripoti WHO iliyotolewa na PRB (Population Reference Bureau), idadi ya watu wanaoishi na shinikizo la damu iliongezeka maradufu kati ya mwaka 1990 na 2019, kutoka milioni 650 hadi bilioni 1.3.

Utafiti wa sababu 87 za kitabia, kimazingira, kikazi na kimetaboliki ulibaini kuwa shinikizo la juu la damu lilikuwa sababu inayoongoza kusababisha vifo vya mapema duniani, vinavyokadiriwa kufikia milioni 10.8 kila mwaka. Likiongoza sababu zingine kuu za hatari kama  matumizi ya tumbaku na sukari ya juu kwenye damu.

Kwa sasa, miongoni mwa watu wazima wenye umri wa miaka 30–79 walio na shinikizo la damu ni asilimia 54 pekee waliogunduliwa, asilimia 42 wanapokea matibabu na asilimia 21 wanachukuliwa kuwa na shinikizo la damu lililodhibitiwa.