
Shinikizo la damu ni tatizo la kiafya linalojitokeza wakati presha ya damu katika mishipa inakuwa juu kupita kiasi.
Kwa wagonjwa wa kisukari, hatari ya kupata shinikizo la damu, inaweza kuongeza uwezekano wa matatizo makubwa ya kiafya kama magonjwa ya moyo, kiharusi na matatizo ya figo.
Shinikizo la damu ni hali ambapo presha ya damu inazidi kiwango cha kawaida cha 120/80. Wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kuhakikisha presha yao inakuwa chini ya 130/80 ili kupunguza hatari ya matatizo ya kiafya. Shinikizo la damu hutokea pale ambapo nguvu ya msukumo wa damu kwenye kuta za mishipa ni kubwa kupita kiasi, hali inayoweza kusababisha uharibifu wa mishipa ya damu na viungo muhimu.
Kwa wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu linaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo mkusanyiko wa mafuta mwilini, uzito mkubwa au unene kupita kiasi na kuongeza mzigo kwenye moyo na mishipa ya damu.
Ulaji wa chumvi kupita kiasi huongeza kiwango cha maji mwilini, hali inayoongeza shinikizo la damu. Ukosefu wa mazoezi, hupunguza uwezo wa moyo na mishipa ya damu kufanya kazi kwa ufanisi.
Msongo wa mawazo wa mara kwa mara huongeza presha ya damu. Wagonjwa wa kisukari wana hatari ya kupata matatizo ya figo, ambayo yanaweza kusababisha shinikizo la damu.
Tabia ya uvutaji sigara na unywaji pombe huongeza msukumo wa damu na kuharibu mishipa ya damu.
Shinikizo la damu halina dalili dhahiri, na wengi hujua tatizo hili baada ya kupimwa. Hata hivyo, dalili zinazoweza kujitokeza ni pamoja na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara, kizunguzungu, uchovu usio wa kawaida, kelele masikioni, kutokwa na jasho jingi na tatizo la kutoona vizuri.
Shinikizo la damu linaweza kusababisha madhara kwa wagonjwa wa kisukari, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa hatari ya mshtuko wa moyo, matatizo ya figo, yanayoweza kusababisha kushindwa kwa figo.
Kupungua kwa uwezo wa kuona au upofu, hatari ya kupooza kutokana na kiharusi, uharibifu wa mishipa ya damu, unaoweza kusababisha ugonjwa wa moyo wa muda mrefu
Kwa wagonjwa wa kisukari, kudhibiti shinikizo la damu ni jambo muhimu ili kuepuka matatizo ya kiafya kwa kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi na chumvi nyingi.
Kula matunda, mboga, nafaka zisizokobolewa, na protini zisizo na mafuta mengi. Tumia angalau dakika 30 kila siku za kufanya mazoezi ya mwili kama kukimbia, kutumia mbinu za kupunguza msongo wa mawazo kama vile kufanya mazoezi ya kupumua, kutembea, na kushiriki katika shughuli unazozipenda.
Pia acha uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe na kupima shinikizo la damu mara kwa mara.