Shigella: Kampuni za madini zinalazimika kuiuzia BoT asilimia 20 ya dhahabu

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amezitaka kampuni kubwa za uchimbaji madini zinazofanya kazi mkoani humo kutii sheria inayozitaka kutenga asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa na kuiuza kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akizungumza leo Aprili 11, 2025 wakati wa kusaini mkataba wa utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kati ya kampuni ya Bucreef na Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Shigella amesema tayari wachimbaji wadogo wameitikia agizo hilo, lakini kampuni kubwa zinasuasua kutekeleza sheria hiyo.

“Hatuwezi kutunga sheria halafu hatuikusanyi dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa, tunakimbizana na wadogo. Sheria hii ni kwa wote wanaosafirisha dhahabu nje ya nchi. Unataka kusafirisha utapewa kibali cha asilimia 80 na hiyo 20 unapaswa kuiuzia BoT,” amesema Shigella.

Ameipongeza Wizara ya Madini kwa kutilia mkazo suala hilo na kuitaka iendelee na msimamo huo ili utekelezaji wa sheria hiyo ufanye kazi kwa kampuni kubwa kama vile Barrick, GGML na Bucreef, ili kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali zake kwa haki.

Oktoba mosi 2024, Tume ya Madini ilitoa tangazo linalowataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kutekeleza takwa la sheria ya madini ya mwaka 2019, linataka kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia BoT.

Serikali ilianzisha utaratibu wa kununua dhahabu ukiwa ni mpango mkakati wa kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni, ambapo kila mwaka Serikali inalenga kununua tani sita za dhahabu.

Ataka CSR itekelezwe

Akizungumzia miradi ya CSR, Shigella amesisitiza kuwa utekelezaji si wa hiari bali ni wa kisheria, hivyo kampuni husika zitekeleze bila usumbufu wala ujanjaujanja.

“Sheria ya madini haikutungwa kwa ajili ya kufurahishana, bali kuleta matokeo chanya, hii ni hiari ya ulazima yaani ni wajibu wa lazima,  zipo kampuni zinafanya vizuri lakini zipo ambazo zinasumbua na hii ni kwa sababu wana ujanjaujanja,” amesema Shigella.

Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buckreef, Isaka Bisansaba amesema mgodi huo utaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

“Tunatarajia kuona miradi hii inaleta mageuzi chanya katika maisha ya wananchi na sisi kama mgodi tutaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha fedha hizi zinaleta matokeo makubwa ya maendeleo,” amesema.

Katika hafla hiyo, miradi ya CSR yenye thamani ya Sh422 milioni imesainiwa kwa ajili ya kutekelezwa katika sekta ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.

Mwaka jana, miradi mingine yenye thamani ya Sh400 milioni ilisainiwa na asilimia 90 ya utekelezaji wake tayari umekamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *