
Kitoto cha 2000, Lamine Yamal, kimekuwa gumzo duniani tangu kitambulishwe na timu yake ya Barcelona kikiwa na miaka 16 mwaka jana.
Kwa sasa Lamine Yamal ana miaka 17 na ameshavunja na kuweka rekodi takribani 20 za umri mdogo.
Bila shaka unakumbuka wakati wa Euro 2024 pale alipokuwa akivunja kila rekodi, hadi timu yake (Hispania) ikatwaa ubingwa.
Aliingia kwenye mashindano akiwa na miaka 16 na akatoka akiwa na miaka 17. Juma lilipopita, akiwa na miaka 17 na siku 105, Lamine Yamal aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga bao kwenye El Clasico, alipoiongoza Barcelona kuisambaratisha Real Madrid 4-0 Santiago Bernabeu.
Mafanikio ya Lamine Yamal yamehamasisha watoto wengi na wazazi wao kuongeza bidii ili siku moja iwe upande wao.
Bahati mbaya ni kwamba nchini Tanzania, mamlaka zetu za soka hazijahamasika hata kidogo kumzalisha Lamine Yamal wake.
Hii inathibitishwa na sheria zinazotumika kuendesha mashindano yetu. Hivi sasa ligi za vijana chini ya miaka 17 na 20 zinaendelea.
Cha ajabu ni kwamba sheria za mashindano haya haziruhusu wachezaji wa umri mmoja kushiriki mashindano ya umri mwingine hata kama umri wake unaruhusu.
Yaani mchezaji mwenye miaka chini ya 17 haruhusiwi kushiriki mashindano ya umri wa chini ya miaka 20.
Sijui kama hapo tumeelewana!?
Ni hivi…
TFF kama waandaaji wa mashindano hayo wameweka sheria kuwakataza wachezaji wa chini ya miaka 17 kushiriki ligi ya chini ya miaka 20.
Chini ya miaka 17 ni kuanzia miaka 16 kushuka chini. Na chini ya ni kuanzia 19 hadi 17.
Kwa hiyo kwa mujibu wa kanuni za TFF, mchezaji mwenye miaka 16 haruhusiwi kushiriki ligi ya chini ya miaka 20 hata kama uwezo unaruhusu.
Yaani hata kama timu fulani imefanikiwa kumpata Lamine Yamal wake, basi haitoruhusiwa kumtumia kwenye mashindano ya chini ya miaka 20.
Hii ni sheria ya hovyo sana. Hivi endapo na wenzetu wangekuwa na sheria kama hizi tungewaona akina Lamine Yamal, Ansu Fati au Pau Cubarsí?
Kwenye mpira umri wa mchezaji haujawahi kuwa tatizo endapo uwezo upo. Hata kama mchezaji ana miaka 15, kama ana uwezo anaruhusiwa kucheza hata timu ya wakubwa, achilia mbali timu ya umri wa juu yake.
Kwenye ligi ya Marekani (MLS), Cavan Sullivan wa Philadelphia Union alicheza mechi yake ya kwanza na timu kubwa akiwa na miaka 14 na siku 293.
Ethan Nwaneri wa Arsenal ya England alicheza mechi yake ya kwanza na timu kubwa akiwa na miaka 15.
Martin Odegaard alichezea timu yake ya taifa ya Norway kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 16.
Wakati wenzetu wanaruhusu wachezaji wao wa umri kama huo kuchezea timu kubwa, sisi tunawazuia kuchezea timu za vijana wa umri wa juu yao kidogo tu…shida sana!
Bahati mbaya waliotunga kanuni hawakusema walilenga kufikia nini kwenye hili, lakini hata kama walilenga kitu, bado hii ni sheria ya hovyo.
Namtumia sana Lamine Yamal kwa sababu ndiye mchezaji aliyeng’aa zaidi kipindi hiki akiwa na umri mdogo sana.
Akiwa na miaka 16 na siku 57, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuichezea na kuifungia bao Hispania.
Akiwa na miaka 16 na siku 87, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye La Liga.
Akiwa na miaka 16 na siku 338, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza kwenye Euro.
Akiwa na miaka 16 na siku 362 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga kwenye Euro.
Akiwa na miaka 17 na siku moja, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda ubingwa wa Euro.
Haya yote yasingewezekana endapo angekuwa Tanzania maana sheria zetu zingemkandamiza na kuzuia kipaji chake kung’aa.
Tubadilike!