Sheikh Qassem: Hizbullah kulenga Tel Aviv kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya Beirut

Kiongozi wa Hizbullah amesema harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon iko tayari kupigana vita vya muda mrefu dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, na kwamba jibu lao kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya anga dhidi ya Beirut litakuwa kulenga katikati mwa Tel Aviv.

Sheikh Naim Qassim alisema hayo katika hotuba yake ya televisheni siku ya Jumatano, akizungumzia mashambulizi ya kikatili ya Israel katika wilaya tatu za katikati mwa Beirut katika siku za hivi karibuni, mojawapo ikiwa ni shahidi mkuu wa vyombo vya habari wa Hizbullah Mohammad Afif na wanachama wanne wa timu yake.

Sheikh Qassim alisema kuwa utawala huo ulimuua shahidi Afif alipokuwa “katika eneo la kiraia, vyombo vya habari na kisiasa ambalo linapaswa kulindwa katika kesi kama hizo.”

“(Israel) ilishambulia, kuua na kulenga kitovu cha mji mkuu Beirut, kwa hivyo lazima watarajie kuwa jibu litakuwa katikati ya Tel Aviv. Hatuwezi kuondoka katika mji mkuu chini ya mapigo ya adui Israeli isipokuwa kwa kumlazimisha alipe gharama. “

Sheikh Qassim amerejelea uwezo wa Hezbollah katika kushughulikia mizozo, akisema kwamba baada ya mauaji ya Sayyed Hassan Nasrallah, imelichukua kundi hilo siku kumi tu kupona.

Amesema harakati hiyo imejitayarisha kwa vita vya muda mrefu dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Amepongeza kusimama kidete kwa muqawama katika kukabiliana na uvamizi wa Israel, akibainisha kwamba mashambulizi ya kulipiza kisasi ya kundi hilo yamewafanya mamia ya walowezi kuhama na kutoka katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu.

Mkuu huyo wa Hizbullah amesema licha ya hali ya machafuko nchini Lebanon, kundi hilo la muqawama litaendelea kuwaunga mkono Wapalestina huko Gaza.